Vijana wenye Ualbino wahamasishwa kujiunga na Elimu ya Ufundi Stadi
Last Update on:2017-09-15 06:19:00

Vijana wenye ualbino, pamoja na ulemavu mwingine wamehamasishwa kutumia fursa mbalimbali za elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kupata ujuzi wa kuwasaidia kuajirika na kushiriki kikamilifu katika kuchangia kwenye maendeleo ya kiuchumi nchini.

Akiwasilisha mada kuhusu Fursa za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika warsha iliyowakutanisha vijana wenye ualibino September 7, 2017, Afisa Uhusiano wa VETA Dora Tesha alisema kuwa VETA imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha fursa sawa za mafunzo kwa makundi yote kwenye jamii ikiwemo watu wenye mahitaji maalum.

Akitoa mfano, alisema katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia 2010 hadi 2015 vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi vilidahili wanafunzi wenye wenye ulemavu 3701, miongoni mwao 1730 wakiwa wanaume na 1971wanawake. Asilimia kubwa (57%) ya wanafunzi hao walikuwa ni wenye ulemavu wa viungo wakifuatiwa na viziwi (23%).

Alisema idadi ya watu wenye ualbino katika vyuo vya ufundi stadi bado ipo chini huku takwimu zikionesha kuwa kwa mwaka 2012 hadi 2016 idadi ya watu wenye ulemavu waliosajiliwa kwenye vyuo vya ufundi stadi walikuwa 4492 kati yao wenye ualbino ni 420 pekee.

Alizitaja baadhi ya sababu za udahili wa watu wenye ualbino kuwa wa chini kuwa ni pamoja na kukosekana kwa uelewa kuwa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ni kwa makundi yote ya jamii, ukosefu wa ujasiri kwa watu wenye ualbino na mtazamo wa jamii juu ya kundi hilo kuingia kwenye mfumo rasmi wa ajira na kukosekana kwa watu wa mfano (Role models) katika elimu ya ufundi stadi kutoka kwenye kundi hilo.

Naye, David Edward Afisa Uhusiano pia kutoka VETA aliwasihi vijana wenye ualbino kuwa mabalozi kwa wenzao juu ya umuhimu wa kujipatia ujuzi ili waweze kuendesha maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa.

Msimamizi wa warsha hiyo kutoka shirika la Under The Same Sun Josephat Igembe alisema mada hiyo imetoa mwanga na kufungua uelewa wa vijana hao juu ya fursa za kujipatia ujuzi na kwamba wataitumia vyema.

Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo Paskazia Yahaya kutoka mkoani Morogoro alisema kuwa mada ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi imemsaidia kutambua kuwa fursa ya kujipatia ujuzi ni pana sana kwa kuwa si lazima mwanafunzi ahudhurie masomo chuoni kwani kuna njia nyingi za kutoa mafunzo.

“Nimehamasika sana kwenda VETA kupata ujuzi ili niweze kujiajiri mwenyewe kwa kuwa changamoto ya kuajiriwa imekua kubwa sana,” Alisema.

Warsha hiyo iliratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la Under the Same Sun kwa lengo la kuwajengea uelewa vijana wenye ualbino nchini kuhusu masuala na mifumo mbalimbali ya kielimu na ajira nchini na ilihudhuriwa na vijana zaidi ya 70 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Search News Post
Home Remedies For Wrinkles