VETA yapokea magari kwa ajili ya kuboresha mafunzo
Last Update on:2017-10-30 08:20:00

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Dar es Salaam imepokea magari tisa yaliyotumika kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) kwa ajili ya kuendeshea mafunzo.

Akikabidhi magari hayo Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la EGPAF Bi Jacquesdol Massawe alisema kuwa EGPAF imewiwa kutoa msaada wa magari hayo kwa VETA ili kuwezesha uboreshaji wa mafunzo katika vyuo vya Ufundi Stadi

. Alisema shirika lake linatambua mchango mkubwa wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa taifa kwa kuwa vijana wengi wamekuwa wakifaidika na mafunzo hayo ambayo yanawawezesha kwa kiasi kikubwa kuajirika.

Alisema mahusiano mazuri kati ya VETA na EGPAF yanatarajiwa kuzaa matunda mengi zaidi na kwamba shirika lake litaendeleza ushirikiano huo ili kunufaisha vijana wengi zaidi.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam Habibu Bukko alisema kuwa magari hayo yamekuja wakati mwafaka ambapo VETA inakabiliwa na upungufu wa magari kwa ajili ya kufundishia na kwamba upungufu huo unasababishwa na Sheria za Manunuzi ambazo haziruhusu ununuzi wa magari yaliyotumika.

Alisema magari hayo yanayokadiriwa kuwa na thamani ya Shilingi Milioni 90 yatapunguza kwa kiasi kikubwa uhaba uliopo na hivyo kuboresha utoaji wa mafunzo katika fani zinazohusiana na magari.

Bukko aliwaomba wadau mbalimbali kushirikiana na VETA katika kufanikisha juhudi zake za utoaji wa mafunzo bora kwa kusaidia vifaa mbalimbali vya utoaji mafunzo na kwamba misaada inayohitajika si magari pekee.

Akitoa shukrani zake kwa shirika hilo, Mkuu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam Douglas Kipokola alisema chuo chake kitahakikisha kuwa magari hayo yanatumika kikamilifu kuongeza wigo wa utoaji mafunzo hasa kwa fani ya udereva na ufundi magari.

Alisema mgao wa magari ambayo chuo chake kitapewa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa udereva. EGPAF - Tanzania

Search News Post
Home Remedies For Wrinkles