VETA Shinyanga yaanzisha kozi ya ufundi wa mitambo mikubwa
Last Update on:2018-02-22 10:17:00

Chuo cha ufundi stadi VETA Mkoani Shinyanga, kimezindua mafunzo mapya ya ufundi wa Mitambo Mikubwa (Heavy Duty Equipment Mechanics), mafunzo ambayo yatasaidia vijana wengi kupata ajira kwa urahisi ndani ya Migodi na katika shughuli za ujenzi wa barabara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kozi hiyo tarehe 19 Februari 2018 kwenye chuo cha VETA Shinyanga, Kaimu Mkurugenzi wa Soko la Ajira, Mipango na Maendeleo wa VETA, Hildegardis Bitegera alisema kuwa kozi hiyo imeanzishwa baada ya utafiti wa soko la ajira kubaini uhitaji mkubwa wa mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya kusaidia sekta ya madini katika mikoa ya kanda ya ziwa.

Alisema, katika hatua ya awali baada ya utafiti VETA Shinyanga ilianzisha kozi ya Ukataji na Ung’arishaji vito (Gemstone cutting Carving and Polishing) na kufatiwa na kozi ya Uendeshaji wa Mitambo Mikubwa (Plant Operations) na hatimaye kozi ya Ufundi wa Mitambo Mikubwa kwa ufadhili wa Serikali ya Canada chini ya Shirika la CICan kupitia mradi wa Uimarishaji Mafunzo kwa ajili ya Ajira (ISTEP).

“Leo tunawaambia watu, hasa vijana kuwa tuna kozi mpya yenye fursa kubwa ya ajira na kwa hivyo waje wajifunze. Kwa upande mwingine, tunawaambia waajiri, hasa katika upande wa shughuli za uziduzi (extractive) na ujenzi kuwa watarajie kutoka kwetu nguvukazi yenye ujuzi na mahiri kwenye ufundi wa mitambo mikubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa, VETA inatarajia vilevile kuongeza kozi za Uchimbaji, Ulipuaji,na nyingine zinazohusiana na sekta ya madini.

Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga Afridon Mkhomoi, alisema kuwa uanzishwaji wa kozi hiyo umewezekana kwa ushirikiano mzuri wa vyuo marafiki katika utekelezaji wa mradi wa ISTEP ambavyo ni Chuo cha New Caledonia na Chuo cha the Rockies vya nchini Canada.

Alisema, pamoja na mafunzo mengine ya uwezeshaji kwa Menejimenti, Walimu na Wafanyakazi wengine, vyuo marafiki walitoa mitambo na vifaa vingine vya kufundishia kwa ajili ya kozi hiyo.

Aliishukuru Serikali ya Canada na chuo cha College of New Colidonia (CNC) kwa ufadhili walioutoa wa vifaa hivyo vya kujifunzia kutengenezea mitambo ambavyo vimewezesha mafunzo kuanza mara moja.

Alisema, msaada huo ulichangia katika kuanzisha kozi kwa kudahili wanafunzi 20, ambao kati yao 16 ni wa kiume na wanne ni wa kike.

“Natoa wito kwa vijana mkoani Shinyanga kuichangamkia kozi hii mpya ambayo itawapatia ajira kwa urahisi ndani ya migodi kwa kutengeneza mitambo ambayo itakuwa ikiharibika sababu wataalamu wake ni wachache,” alisema.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Thomas Katebalirwe, matarajio ya Serikali ni kupata watalamu wengi wa ufundi wa mitambo hapa nchini.

Aliwaomba VETA kuendesha kwa ufanisi mkubwa kozi hiyo akiamini kuwa baada ya miaka michache chuo cha VETA Shinyanga kitakuwa chuo cha mfano kwa mafunzo yanayohusiana na shughuli za uchimbaji na uchakataji madini.

Aidha mwakilishi kutoka Chuo cha New Colidonia (CNC), Romana Pasca, alisema wameamua kufadhili vifaa kwa ajili ya mafunzo ili Tanzania ipate kuongeza idadi kubwa ya wataalamu wa kutengeneza mitambo kutoka ndani ya nchi, pamoja na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Nao baadhi ya wanafunzi wanaosoma mafunzo hayo mapya akiwamo Calvin Msafiri, waliipongeza Serikali kwa kushirikiana na nchi ya Canada kuanzisha kozi hiyo mpya ambayo wana matumaini kuwa itawapatia ajira kwa urahisi na kuinua uchumi wa maisha yao.

Search News Post
Home Remedies For Wrinkles