Teknolojia ya kisasa yaboresha utoaji mafunzo katika chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi
Last Update on:2018-04-26 09:12:00

Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kimeanza matumizi ya vifaa vya teknolojia ya kisasa ili kuboresha utoaji mafunzo.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Habibu Bukko alisema vifaa hivyo vya kisasa vitaendelea kuongezeka chuoni hapo ili kurahisisha ufundishaji na kuongeza udahili.

“Kwa sasa chuo cha MVTTC kina vifaa vingi vya kisasa vya kufundishia na hivyo kutupa nafasi ya kutoa mafunzo kwa ufanisi zaidi na kuhudumia idadi kubwa zaidi ya wanafunzi wanaohitaji kusomea ualimu wa ufundi stadi” Alisema.

Aliwasihi mafundi stadi kujitokeza kwa wingi kusomea ualimu katika chuo hicho kwa kuwa vyuo vingi vya ufundi stadi vinatarajia kujengwa nchini na kwamba vinahitaji walimu wa kutosha kuvihudumia.

Alitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni vifaa viwakilishi (Simulators) vya kufundishia fani ya Umeme wa Majumbani na Viwandani ambavyo vimeshafungwa na vitaanza kutumika kwa kuwafundishia Waalimu Wanafunzi na Wanafunzi wa Ufundi Stadi wa fani ya Umeme.

Vingine ni vifaa vya kufanyia mikutano na kutolea mafunzo kwa njia ya Video ambavyo kwa sasa vinawezesha mikutano na mafunzo ya masafa kati ya Chuo cha MVTTC na Chuo cha VETA cha Mkoa wa Dodoma pamoja na vifaa vilivyofungwa maabara ya lugha (Language lab) ili kukuza uwezo wa wanafunzi kutumia lugha ya Kingereza na Kifaransa.

Alisema chuo hicho pia kipo kwenye hatua za mwisho za kuanzisha mafunzo kwa njia ya masafa ili kufundisha taaluma ya Ualimu wa Ufundi Stadi kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano na kwamba mpango huu unatarajiwa kuzinduliwa mwaka huu.

Kuhusu uwezo wa waalimu kutumia vifaa hivyo vipya vya teknolojia Bukko alisema siyo changamoto kwa kuwa walimu wana utaalamu wa ufundi stadi kwa muda mrefu na kwamba wana uwezo wa kujifunza na kuelewa kuhusu matumizi yake kwa muda mfupi tu.

Mwalimu wa fani ya Umeme chuoni hapo Annelisa Andengulile alisema kuwa kuja kwa vifaa hivyo vinawawezesha kumwelewesha mwanafunzi kuelewa zaidi.

Amesema kuwa matumizi ya vifaa hivyo yatamsaidia kwa kiasi kikubwa kuwafundisha wanafunzi kwa urahisi na kuwawezesha kuelewa kwa haraka zaidi tofauti na ilivyokuwa mwanzo alipokuwa akitumia vifaa vya kianalojia.

Amesema ndani ya mwezi mmoja tu toka vifaa hivyo vilivyofungwa katika karakana yake, ameweza kuelewa matumizi yake ya kiasi kikubwa na anaendelea kujifunza zaidi aweze kumudu vyema matumizi yake.

MVTTC ni Chuo pekee cha Umma hapa nchini kinachotoa Elimu na Mafunzo ya Ualimu wa Ufundi Stadi na kwa sasa kina uwezo wa kudahili wanafunzi 440 kwa mwaka.

Mafunzo katika chuo hicho hutolewa kwa ngazi ya Stashahada na Astashahada katika chuo hicho na pia kwenye vituo vya nje ya Chuo (Off-Campus) vipatavyo 13.

Search News Post
Home Remedies For Wrinkles