Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Rukwa waanza rasmi
Last Update on:2018-09-01 06:28:00

Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Rukwa umeanza rasmi baada ya makabidhiano ya mradi huo kati ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo Stadi (VETA) na mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya Tendar International Ltd ya Kichina.

Makabidhiano kati ya VETA na Mkandarasi wa ujenzi huo yalifanyika tarehe 30 Agosti, 2018 wilayani Sumbawanga na kuhudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt Halfan Haule.

Ujenzi wa chuo hicho cha mkoa unatarajiwa kugharimu takribani kiasi cha bilioni kumi (Bil. 10) na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 na umelenga kukidhi mahitaji ujuzi katika mkoa wa Rukwa na maeneo ya jirani.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi VETA Adelina Macha amesema dhamira ya VETA ni kujenga vyuo vya ufundi stadi kila mkoa ili kuongeza udahili na uendelezaji ujuzi, hivyo kwenda sambamba na kasi ya utekelezaji wa mkakati wa serikali kuelekea kwenye uchumi wa viwanda,

kwani VETA ina jukumu kubwa katika kuandaa nguvukazi kwa ajili ya uchumi viwanda. Macha amesema miongoni mwa vyuo vya hadhi ya mkoa ambavyo viko mbioni kujengwa ni pamoja na Njombe, Geita, Simiyu, pamoja na Rukwa.

Akizungumza kuhusu chuo hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Soko la Ajira VETA, Hildergardis Bitegera amesema kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 600 kwa mwaka kwa ngazi ya kwanza hadi ya tatu katika mafunzo ya muda mrefu na wanafunzi wasiopungua 900 kwa mafunzo ya muda mfupi.

Amesema kuwa ujenzi huo utahusisha ujenzi wa karakana zitakazofundisha mafunzo kwa vitendo katika kozi za ufundi magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, uhudumiaji na uuzaji wa vinywaji, ufundi umeme, uandaaji na utayarishaji wa chakula, mafunzo ya ukatibu muhtasi, ubunifu wa mavazi na ushonaji wa nguo, ufundi useremala , ufundi uashi, ukarimu na utengenezaji wa chakula.

Amesema utafiti wa soko la ajira ulibaini kuwa shughuli kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa ni kilimo, ufugaji na uvuvi, hivyo miongoni mwa kozi zinazotarajiwa kufundishwa ni usindikaji wa chakula ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt Halfan Haule amesema kuwa Mkoa wa Rukwa ulikuwa na uhitaji wa Chuo cha mafunzo ya Ufundi Stadi kwa muda mrefu, hivyo kuanza ujenzi huo kunaleta matumaini makubwa kwa vijana na wananchi wengine mkoani humo kupata fursa za mafunzo ya ujuzi katika eneo la jirani nao.

Aliishukuru serikali kwa kuupa kipaumbele mkoa wa Rukwa na kuamua kujenga chuo cha Mkoa cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi.

Aliongeza kuwa matarajio ya serikali ni kuwa uwepo chuo hicho kutahamasisha maendeleo na kuongeza kipato kwa wanacnhi katika mkoa wa Rukwa ambapo watafanya usindikaji wa chakula pamoja na uhifadhi wa mazao.

Search News Post
Home Remedies For Wrinkles