Ole Nasha: Wahitimu vyuo vya elimu ya juu sasa wanakimbilia ufundi stadi
Last Update on:2018-10-09 10:23:00

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amewataka vijana na umma wa Watanzania kwa ujumla kutambua umuhimu na kutumia fursa za mafunzo ya ufundi stadi, kwani fani hizo sasa zinahitajika zaidi nchini, hivyo hata wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu sasa wanakimbilia kujifunza ufundi stadi.

Akiongea baada ya kutembelea chuo cha VETA Manyara, Jumatatu, tarehe 8 Octoba, 2018, Ole Nasha alisema sasa kuna msukumo mkubwa wa elimu ya ufundi kuliko wakati mwingine wowote kutokana na mwelekeo wa kiuchumi pamoja na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii nchini.

Alizitaka sababu mahsusi zinazoipa umuhimu mkubwa elimu ya ufundi kuwa ni pamoja uhitaji wa nguvu kazi ya ufundi kwenye uchumi wa viwanda na uwekezaji mkubwa wa serikali kwenye ujenzi wa miundombinu mbalimbali.

“Viwanda viko vingi, vidogo, vya kati na vikubwa lakini vyote vina sifa moja, vinahitaji nguvukazi mahiri ya ufundi. Lakini sote ni mashahidi kuhusu uwekezaji wa serikali kwenye miundombinu, ikiwemo ujenze wa reli ya kisasa ya kutumia umeme (standard gauge). Uwekezaji wa miundombinu kama ile hauwezi ukaenda bila ya mafundi. Uuwekezaji ambao unahitaji mafundi si kwa ajili ya ujenzi pekee bali hata katika matengenezo mengine baada ya kukamilika kwake,” alisema.

Alitoa mfano mwingine wa uwekezaji mkubwa unaohitaji mafundi ni ule wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania ambalo ujenzi wake unatarajiwa kutoa fursa nyingi kwa mafundi.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni urahisi mkubwa kwa wahitimu wa ufundi kupata ajira, kwa kuwa na fursa kubwa za kuajiriwa au kujiajiri, huku akiwataka wanafunzi wa VETA kujiona wamechagua njia sahihi na yenye manufaa makubwa kwao.

“Kwa hiyo kwanza jiondoeni unyonge kwamba mimi nasoma VETA tu, lakini mwenzangu kaenda chuo kikuu. Kwa taarifa yenu, mna nafasi kubwa ya ajira kuliko mtu ambaye ameenda chuo kikuu. Miaka ya karibuni tumeanza kuona wimbi kubwa la wanafunzi waliomaliza chuo kikuu wakija kuomba kujiunga VETA. Mimi nimekutana nao wengi, ukimuuliza anasema nimekwenda kujifunza nadharia lakini sijaona kitu ilichonisaidia. Ninyi mnafahamu nadharia na vitendo,” alifafanua.

Katika hafla hiyo baadhi ya wanafunzi wa VETA Manyara waliiomba serikali kuweka utaratibu wa kuwasaidia wahitimu wa ufundi stadi kupata vifaa ili waweze kujiajiri, huku mwanafunzi Matheo Masoye wa mwaka wa pili fani ya Umeme akiiomba serikali kuandaa mazingira mazuri kwa watu wenye ulemavu nao kupata elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili pia wajikwamue kiuchumi.

Akijibu hizo Ole Nasha aliitaka VETA kuhakikisha kuna mazingira ya kuwawezesha wenye ulemavu nao kupata fursa za mafunzo ya ufundi stadi kama ilivyo kwa watu wengine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt Pancras Bujulu alishauri kuanzisha mfuko maalum (revolving fund) katika halmashauri kwa ajili ya kuwasaidia wahitimu wa ufundi stadi vifaa na mahitaji mengine ya kuwawezesha kujiajiri.

“kwa sababu shughuli hizo zinazalisha, wapewe utaratibu wa kulipa ili na wengine wanufaike,” alisema.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliambatana viongozi na maafisa wengine wa wilaya ya Babati akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Simon Kitundu, Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul na Mbunge wa Babati Vijijini Virajlal Jituson na alikutana pia na Wajumbe wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi pamoja na Menejimenti na wafanyakazi wa VETA kutoka Makao Makuu, VETA Kanda ya Kaskazini na Chuo cha VETA Manyara.

Search News Post
Home Remedies For Wrinkles