The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Finland yafadhili mabinti 240 kusoma kozi fupi VETA.
Posted on: Friday, 24 March 2023
Serikali ya Finland kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania umetoa ufadhili kwa mabinti 240 kupata mafunzo ya ufundi stadi kupitia programu ya Chaguo Langu Haki Yangu.
Mabinti wanaofadhiliwa ni wale wanaotoka kwenye mazingira magumu, ikiwemo waliofanyiwa ukatili na kupewa mimba za utotoni na wenye ulemavu. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo ni katika Mikoa miwili ya Mara na Shinyanga katika Wilaya za Kishapu, Kahama na Butiama.
Akizungumza jana, tarehe 23 Machi 2023, wakati wa ufunguzi wa programu hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude, amewapongeza wadau hao kwa ufadhili walioutoa, akisema mafunzo hayo yatawawezesha mabinti waliofadhiliwa kutimiza ndoto zao zilizotaka kukatishwa kutokana na changamoto walizopitia.
Vilevile, Mhe. Mkude alimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa kipaumbele kwenye elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kutoa fedha kwa ajili ya kujengwa vyuo vya ufundi stadi VETA ngazi ya wilaya ikiwemo Wilaya ya Kishapu.
Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Ndugu Abdallah Ngodu akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA, amewaomba wadau hao kupanua zaidi programu hiyo kwa kuwa VETA ina vyuo nchini kote, vikiwa na fani zipatazo 90.
“Tunaweza kutumia fursa ya vyuo hivi kuwapatia mabinti wengi zaidi mafunzo kama haya, hasa kwa kuzingatia hali ya udahili wa wasichana kwenye vyuo vya VETA kwa sasa bado ni ndogo ukilinganisha na wavulana,” amesema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ubalozi wa Finland, Ndugu Juhana Lehtinen, amesema wamefarijika kuona namna mabinti hao wanavyopata mafunzo ya ufundi stadi ambayo yanategemewa kubadilisha mfumo wa maisha yao.
"Tumekuja hapa VETA wilayani Kishapu kuona namna utekelezaji wa mradi wa Chaguo Langu Haki Yangu unavyotekelezwa na kusaidia mabinti ambao wamefanyiwa ukatili na wengine kupewa mimba za utotoni…nimefurahi kuona unatekelezwa vyema na mabinti wanapata ujuzi," amesema
Naye Mshauri wa masuala ya jinsia kutoka UNFPA ambao ni waratibu wa programu hiyo, Maya Hansen, amewataka mabinti hao kutumia vyema fursa waliyoipata kuleta chachu ya mabadiliko katika maisha yao na kutofanya changamoto walizopata mwanzo kuwarudisha nyuma.
Mkurugenzi wa Shirika la WILDAF Tanzania, Anna Kulaya, amesema kazi kubwa ya WILDAF ni kutetea haki za wanawake na wasichana, hivyo programu hiyo imekuja wakati mwafaka na itasaidia kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kupitia ujuzi ambao utawasidia kuendesha maisha yao bila utegemezi.
Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Ndugu Magu Mabelele, ambaye pia ni msimamizi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Kishapu, amesema walipokea mabinti 240 kupitia Shirika la WiLDAF kutoka Hamashauri tatu za Wilaya za Kishapu, Kahama na Butiama na hivyo uongozi wa chuo cha VETA Shinyanga ukaamua kuwagawa mabinti hao kutokana na fani walizochagua ambapo mabinti 171 wanapata mafunzo katika fani za Ushonaji (101), Ufundi Bomba (11), Saluni (37), pamoja Ufundi Umeme (22).
Wengine 69 wamesalia katika chuo cha VETA Shinyanga ambapo wanasomea fani za Uhazili na Tehama (27), Upishi (18), Uchomeleaji na Uungaji Vyuma (7), Ufundi wa Magari (3) pamoja Udereva wa Magari na Mitambo