Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Fortunatus Musilimu amewataka madereva nchini kuchangamkia fursa za mafunzo ya udereva bora katika vyuo mbalimbali ikiwemo vyuo vya VETA.
Akizungumza wakati wa mahafali ya mafunzo ya muda mfupi katika Chuo cha VETA Dar es Salaam Kamanda Musilimu alisema zoezi la ukaguzi wa vyeti kwa madereva litafanyika kama ilivyopangwa ambapo baada ya miezi mitano iliyotolewa na Jeshi la Polisi kwa madereva kurudi shuleni na kupata vyeti kumalizika, hakutakuwa na mjadala tena bali hatua stahiki zitachukuliwa.
“Nawakumbusha madereva kuwa mwezi mmoja umeisha katika ile miezi mitano iliyotolewa…. Nawasihi tena kutumia vizuri muda uliobaki wakasome…”Alisema
Alisema vyeti vyote vitatakiwa kuwa na sahihi ya Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa ili kuhakikisha hakuna udanganyifu katika upatikanaji wa vyeti hivyo.
Kamanda Musilimu aliwaasa vijana waliohitimu mafunzo katika chuo cha VETA kuhakikisha wanatumia vyema ujuzi walioupata kuanzisha shughuli zao za kujiingizia kipato kulingana na fani walizosoma.
Naye Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Stella Ndimubenya aliwataka vijana kutumia vyema fursa zinazopatikana katika Halmashauri zao kuwa kuna fungu maalum kwa ajili ya kuwawezesha vijana kufanya shughuli za ujasiriamali wakiwa kwenye vikundi.
Awali, Mkuu wa Chuo hicho Douglas Kipokola alisema chuo chake kwa kushirikiana na chuo cha VETA Kihonda wamejipanga vyema kutoa mafunzo ya udereva bora kwa madereva wote wataohitaji kupata mafunzo hayo.
Alisema hivi karibuni chuo hicho kimeanza kutoa mafunzo kwa madereva wa magari makubwa/malori yanayobeba mizigo na kwamba mtaala wake umeshapitishwa ambapo mafunzo hayo yameanza kutolewa tarehe 3 Septemba mwaka huu huku kukiwa na madereva 30 wanaopata mafunzo kwa wamu ya kwanza.
Kipokola alisema katika mahafali hayo,jumla ya wanafunzi 1125 wamehitimu mafunzo ya muda mfupi na katika fani mbalimbali ikiwepo Udereva, Uendeshaji wa hiteli, uhazili, umeme, compyuta, mapishi, Nywele na urembo na ufundi wa magari.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office