The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Chuo cha VETA Kasulu kimezindua rasmi mpango wa kuwajengea stadi za ufundishaji mafundi mahiri kutoka viwandani na maeneo mengine ya kazi, ili waweze kutoa mafunzo bora ya ufundi stadi kwa vijana kupitia Mpango wa ushirikiano kati ya VETA na Mafundi Mahiri.
Mafunzo ya awali kwa kupitia mpango huo yamewahusisha mafundi mahiri 15 na yamefadhiliwa na Shirika la Maendeleo Enabel kupitia mradi wa Wezesha Binti, na yanalenga mafundi kutoka stadi za Ufundi Magari; Ufundi Ushonaji, Ubunifu na Teknolojia ya Nguo; Ufundi Umeme na Ufundi Bomba.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, tarehe 5 Mei 2025, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Magharibi, Asanterabi Kanza, alipongeza mpango huo, akisema utasaidia kuwezesha wanafunzi wawapo sehemu za kazi kupata mafunzo bora kupitia kwa mafundi mahiri.
“Nawapongeza kwa hatua hii muhimu ya kuanzisha na kupokea mpango huu wa kuwajengea uwezo mafundi mahiri. Pia ninatoa shukrani kwa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kwa kutupatia mkufunzi aliyebobea wa kuendesha mafunzo haya ambayo yatawasaidia mafundi hawa kuwa walimu wa ufundi stadi kwa wengine,” Amesema.
Awali, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kasulu, Bw. Dhabahu Mafwele, amesema mpango huo umeandaliwa kwa kutambua mchango mkubwa wa mafundi walioko kazini katika utoaji wa ujuzi kupitia programu kama Mafunzo kwa Njia ya Kazi (Work-Based Training), Mazoezi kwa Wanafunzi Mahala pa Kazi (Field Attachment), na Mfumo wa Mafunzo ya Uanagenzi (Dual Apprenticeship Training).
Kwa mujibu wa Mafwele, mafunzo hayo yatadumu kwa siku tano na yataendeshwa na mkufunzi mahiri kutoka MVTTC Morogoro, Rogers Sabuni.
“Washiriki watafundishwa mbinu bora na shirikishi za kufundisha kwa kuzingatia mfumo wa CBET (Competence-Based Education and Training), uimarishaji wa maadili ya kazi, usimamizi wa mafunzo kazini (field supervision), utoaji wa mrejesho chanya kwa wanafunzi, pamoja na umuhimu wa ushirikiano kati ya waajiri na VETA kwa uendelevu wa mafunzo ya vitendo,” amefafanua Mafwele.
Amesema, matarajio ya mafunzo hayo ni kuwaona mafundi mahiri, lisha ya utaalamu katika stadi zao, wanakuwa walezi wa kizazi kijacho cha wafanyakazi wenye stadi bora, maadili, uzalendo na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la sasa na la baadaye.