The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam, Wilhard Soko amewaomba viongozi wa Chama cha Mafundi kuhamasisha mafundi kurasimisha ujuzi wao ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za ajira, zabuni na mikopo ya maendeleo.
Akizungumza na viongozi wa Chama Cha Mafundi waliomtembelea ofisini kwake jana, tarehe 27 Aprili 2026, Soko amesema urasimishaji wa ujuzi ni hatua muhimu kwa mafundi kupata vyeti vinavyotambulika rasmi na vinavyoweza kufungua milango ya ajira na kujiajiri.
Amesema jukumu la VETA ni kuwawezesha Watanzania kupata ujuzi wa ufundi stadi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, huku akibainisha kuwa mafundi wenye uzoefu wa angalau miaka miwili wanastahili kushiriki katika zoezi hilo.
“Cheti cha urasimishaji kitamwezesha fundi kuthibitisha ujuzi wake, kushiriki zabuni za serikali, kupata mikopo na kuboresha zaidi ujuzi wake kulingana na mahitaji ya soko,” amesema Soko.
Katika kikao hicho kilicholenga kuimarisha ushirikiano, viongozi wa Chama cha Mafundi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Humphrey Mtenda, walikabidhiwa fomu za usajili kwa ajili ya kuzisambaza kwa mafundi katika wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam.
Viongozi hao wamewahimiza mafundi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, wakisisitiza kuwa zoezi hilo ni la muda mfupi, huku fomu zikitolewa bure pamoja na vyeti vitakavyotolewa baada ya kukamilika kwa taratibu.
Aidha, wameeleza kuwa mpango huo umefadhiliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hatua waliyosema inaonesha kuthamini mchango wa mafundi katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wao, viongozi wa mafundi waliishukuru VETA kwa kutoa fursa hiyo na kuahidi kuhamasisha wanachama wao kuitumia kikamilifu kwa manufaa yao na ya taifa kwa ujumla.