Mhitimu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam, Fidelis Christian Mchana ameibuka mshindi wa kwanza katika kundi la Wabunifu wa Vyuo Vya Ufundi Stadi katika fainali za Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yaliyohitimishwa leo tarehe 7 Machi 2019 katika Viwanja vya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) jijini Dodoma.
Fidelis alishiriki mashindano hayo akiwa na ubunifu wa benchi linaloweza kugeuzwa kuwa meza ya majadiliano na wakati mwingine kuwa meza ya kuchorea (Drawing Table) ambalo katika maonesho hayo watu wamelibatiza jina la Benchi la Maajabu.
Kijana Fidelis amefuatiwa na Mwalimu Emmanuel Bukuku kutoka VETA Dar es Salaam aliyeshika nafasi ya pili na Mwalimu Sussack Mbulu wa VETA Songea aliyeshika nafasi ya tatu.
Mwalimu Emmanuel Bukuku amebuni mfumo wa kutoa ishara ya sauti kwa watumiaji wa barabara wakati Gari Moshi (train) linapokaribia kwenye makutano ya barabara na reli, lengo likiwa ni kusaidia kupunguza ajali zinazotokana na magari au watu kugongwa na Gari Moshi katika makutano ya barabara na reli.
Kwa upande wake, Mwalimu Sussack Mbulu amebuni kifaa cha umwagiliaji (sprinkler) kilicho imara na kinachoweza kuhudumia eneo kubwa na kwa ufanisi mkubwa.
Washiriki wengine kutoka Kundi la Vyuo vya Ufundi Stadi waliofika fainali za mashindano hayo ni Kintu Kilanga (VETA Dar es Salaam) aliyebuni kifaa ya usaili wa watoto wenye ulemavu wa akili; Elly Maduhu (VETA Mara) aliyebuni mashine rahisi ya kuungia vyuma; Aneth Mganga (VETA Kipawa) aliyebuni mfumo wa usalama kwa watumiaji wa pikipiki; Edward Lunyilija (VETA Kigoma) aliyebuni kifaa cha kufukuza mbu; Patrick Jovenary (kutoka Mfumo wa Mafunzo ya Uanagenzi VETA Dar es Salaam) aliyebuni mfumo wa usalama majumbani, kwenye magari na lifti za majumba marefu na Lawrance Mashindano (VETA Mwanza) aliyebuni mashine ya kuzoa na kuchoma magugu maji.
Wakati huo huo, Adam Zacharia Kinyekile wa Songwe naye amekuwa mshindi wa kwanza katika Kundi la Sekta Isiyo Rasmi ambalo VETA pia iliratibu mchakato wa washiriki wa kundi hilo. Adam amebuni mashine au chombo kinachoweza kutoa huduma mbalimbali za kiufundi, uchakataji na usindikaji wa mazao pamoja na huduma zingine mashambani.
Aliyefuatia katika kundi hilo ni Abdul Lwangisa kutoka Gongo la Mboto, Dar es Salaam aliyebuni mashine ya kuchakata takataka ngumu na kutengeneza vipuri vya mashine na vyombo mbalimbali.
Wa tatu katika kundi hilo ni Patrick Mpili akiwakilisha kampuni ya Giant of Genius ambao wametengeneza ingine ya ndege (Jet Engine). Makundi mengine yaliyoshiriki mashindano hayo ni Kundi la Shule za Sekondari (lililoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI); Kundi la Vyuo vya Ufundi Sanifu (lililoratibiwa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam-DIT); Kundi la Vyuo Vikuu na Kundi la Taasisi za Utafiti na Maendeleo (yaliyoratibiwa kwa pamoja na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia-COSTECH).
Akifunga mashindano hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako aliwahimiza wabunifu kujikita zaidi katika kutafuta suluhu za changamoto mbalimbali katika jamii.
Alisema vijana wengi wanaosoma na kuhitimu mafunzo ya ufundi stadi wanaonesha kuwa mahiri na wabunifu katika fani zao akitolea mfano wa baadhi ya vijana (waliohitimu VETA Moshi) kwa kuonesha umahiri na kupata ithibati za kimataifa katika eneo la uungaji vyuma.
Mafunzo yetu ya ufundi stadi yako vizuri na ndio maana serikali imejikita katika kupanua fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi na tunaendelea na ujenzi wa vyuo vya mikoa na wilaya. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Daktari Pancras Bujulu aliwapongeza wabunifu na kusema kuwa VETA ina dhamira ya kusaidia uendelezaji ubunifu katika eneo la ufundi stadi. Aliwahimiza wabunifu kuendelea kutumia vipaji vyao kubuni vitu mbalimbali ili kutatua changamoto mbalimbali katika jamii. “Tumezoea kuagiza vitu kutoka Ulaya, kumbe tunaweza kutengeneza vitu vingi hapahapa,” alisema.
Alisema mchakato wa mashindano ya ubunifu mwaka huu utasaidia zaidi kuwafahamu wabunifu mbalimbali na kuona ni namna gani ya kuwaendeleza na kuwasaidia katika ubunifu wao.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office