The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mkurugenzi Mkuu wa VETA atembelea Chuo cha TEHAMA VETA Kipawa
Posted on: Thursday, 16 November 2023
Mkurugenzi Mkuu wa VETA atembelea Chuo cha TEHAMA VETA Kipawa
Asisitiza ubunifu matumizi ya TEHAMA kutatua changamoto za jamii na kuongeza uzalishaji
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Prosper Mgaya ametembelea Chuo cha TEHAMA cha VETA Kipawa kujionea shughuli za utoaji mafunzo na kuzungumza na wafanyakazi wa chuo hicho.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo leo tarehe 16 Novemba, 2023, jijini Dar es Salaam, Dkt. Mgaya ameagiza Menejimenti na wafanyakazi wa chuo hicho kuongeza ubunifu katika utoaji mafunzo ya TEHAMA na kuhakikisha TEHAMA inatumika kwa ufanisi kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Amesema chuo hicho maalum kwa ajili ya mafunzo ya TEHAMA kinategemewa kuzalisha wahitimu mahiri wenye uwezo wa kutumia ujuzi wao kurahisisha uendeshaji wa shughuli mbalimbali na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
“Msisitizo wangu kwenu ni kuhakikisha mnatoa mafunzo bora, mnafanya ubunifu utakaoweza kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu na kutoa huduma za kitaalamu kwa jamii na kuongeza mapato ya ndani ambayo yatasaidia kupunguza utegemezi wa ruzuku toka serikalini katika kuendesha shughuli za VETA,”amesema
Dkt Mgaya amesema chuo hicho kina fursa kubwa ya kufanya uzalishaji kupitia utoaji wa huduma mbalimbali za TEHAMA kwa jamii inayowazunguka na kuwataka kufanya ubunifu na kutumia vyema fursa hizo ili kujiongezea kipato.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina mategemeo makubwa sana na VETA katika kuwawezesha wananchi kujipatia ujuzi na kuwataka wafanyakazi kutimiza wajibu wao kikamilifu ili kufanikisha azma hiyo.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam, Ndugu Angelus Ngonyani amemshukuru Dkt. Mgaya kwa kutembelea chuo hicho na kuahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa ili kuboresha utoaji mafunzo katika chuo hicho.
Akisoma taarifa ya chuo, Mkuu wa Chuo cha VETA Kipawa, Mhandisi Dickson Mkasanga amesema chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 144 wanaoendelea na masomo kwa kozi za muda mrefu katika fani za TEHAMA, Elektroniki, Umeme wa Majumbani na Umeme wa Viwandani.
Amesema katika kipindi cha mwezi Julai, 2022 hadi mwezi Novemba, 2023 chuo hicho kimetoa mafunzo mbalimbali ya muda mfupi kwa wanafunzi 1,890.
Mhandisi Mkasanga amesema chuo hicho kimejipanga vyema kutoa mafunzo kwenye fani ya mekatroniki ili kuendana na kasi ya ukuaji na uendeshaji wa viwanda na kwamba kwa sasa chuo kina vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufundishia fani hiyo.