The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu aitaka VETA kuanzisha mafunzo ya Usimamizi wa Mnyororo
Posted on: Monday, 28 July 2025
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu aitaka VETA kuanzisha mafunzo ya Usimamizi wa Mnyororo wa taka ngumu
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar, ameitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuanzisha mafunzo ya usimamizi wa mnyororo wa taka ngumu, ili kukabiliana na changamoto kubwa ya usimamizi wa taka inayolikabili maeneo mengi ya miji mikubwa nchini.
Dkt. Omar ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya kikazi katika Makao Makuu ya VETA jijini Dodoma na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Mamlaka hiyo.
Amesema kuwa kwa sasa hakuna chuo chochote nchini kinachotoa mafunzo mahsusi ya stadi za kushughulikia taka ngumu, licha ya kwamba suala hilo limekuwa changamoto kubwa kwa jamii.
“Mnyororo wa taka ngumu unahusisha hatua kadhaa kama uzalishaji wa taka, ukusanyaji, urejelezaji (recycling) na utupaji, na kila hatua ina wahusika wanahitaji kuwa na ujuzi wa kuisimamia kwa ufanisi,” amesema Dkt. Omar na kuongeza kuwa tayari amefanya utafiti kuhusu eneo hilo na kuandaa andiko maalum alilokabidhi kwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, kama rejea ya awali ya kuanzisha mchakato huo.
Mbali na suala la taka ngumu, Dkt. Omar ameshauri VETA kuchangia katika kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo kupitia utoaji wa mafunzo ya teknolojia za umwagiliaji na njia za kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Amesema kazi hiyo inaweza kufanyika kupitia vyuo vya VETA au kupitia kampuni tanzu ya Mamlaka hiyo, Ujuzi Incorporated Co. Ltd.
Aidha, ameihimiza VETA kubuni mradi wa kimkakati kwa ajili ya kuwawezesha wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi kupata ajira, akipendekeza kufuata mfano wa Mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) unaotekelezwa na Wizara ya Kilimo, ambao umeonyesha mafanikio makubwa katika kuwawezesha vijana kupitia sekta ya kilimo.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alimweleza Naibu Katibu Mkuu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo, mafanikio yaliyofikiwa, na mikakati ya baadaye.
Ameeleza kuwa VETA imefanya upembuzi wa mahitaji ya ujuzi nchini (skills mapping), sambamba na kuanzisha kampuni tanzu – Ujuzi Incorporated Co. Ltd.
Amesema upembuzi wa mahitaji ya ujuzi utawezesha kuanzisha programu za mafunzo zinazoendana na mahitaji ya jamii husika na uanzishaji wa kampuni utasaidia kuongeza uzalishaji na kipato.
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Omar ilikuwa na malengo ya kujifunza kuhusu shughuli za taasisi zilizo chini ya Wizara yake, baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kushika wadhifa huo kwenye Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.