The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
PAC YAIMIMINIA PONGEZI VETA KWA UJENZI BORA WA CHUO CHA VETA IKUNGI
Posted on: Friday, 29 March 2024
PAC YAIMIMINIA PONGEZI VETA KWA UJENZI BORA WA CHUO CHA VETA IKUNGI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipa pongezi nyingi Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa ujenzi bora wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ikungi. Mradi huo ulitekelezwa na VETA kwa kutumia nguvukazi za ndani (Force Account).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baada ya kukagua chuo hicho, jana, tarehe 28 Machi 2024, wajumbe wa PAC wameonesha kuridhishwa kwa kiasi kikubwa na ubora wa majengo, miundombinu ya chuo na gharama za ujenzi zilizotumika, huku wakirejea na kuzungumzia tofauti na miradi mingine waliyoitembelea.
“Mmetutia moyo, tumetoka na moyo ulionyooka. Tulikuwa tumesononeka sana baada ya kutembelea miradi mingine iliyojengwa kwa utaratibu huu wa force account,” amesema Makamu Mwenyekiti wa PAC, ambaye pia ni Mbunge wa Vwawa, Mheshimiwa Japhet Hasunga.
Naye Mbunge wa Katavi na mjumbe wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Mhandisi Isack Kamwelwe amesema ametumia muda mwingi kukagua majengo na miundombinu mbalimbali na kubaini kuwa kiwango cha ujenzi wa chuo hicho ni cha ubora wa hali ya juu.
“Mheshimiwa Mwenyekiti (wa PAC), nimezunguka maeneo mengi, kwenye karakana, vyoo na madarasa, kazi hii ni nzuri sana. Kwa force account, kazi hii ni excellent (bora kabisa). Hata majengo yamejengwa kwa spacing (kuacha nafasi), jambo ambalo linasaidia hata kupunguza madhara inapotokea majanga kama moto,” amesema.
Wajumbe wa Kamati hiyo ambayo miongoni mwa majukumu yake ni kutathmini thamani ya matumizi ya fedha za Serikali (Value for money), wamesema kuwa wameridhika kuona kuwa suala la thamani ya matumizi ya fedha limezingatiwa kwa kiasi kikubwa, hasa kwa kuangalia kiwango cha fedha kilichotumika na pamoja na chuo kuanza kudahili wanafunzi.
“Wakati naingia hapa, mimi nilistuka na kudhani kuwa wametumia pesa nyingi sana. Maana nikiangalia majengo yalivyojengwa kwa ubora, magrili kwenye milango na madirisha yalivyo mazito, nikadhani pesa nyingi sana itakuwa imetumika. Nilivyokuja kusikia taarifa kuwa imetumika shilingi 3 tu nimestaajabu sana. Ni kiwango kidoigo sana cha pesa ukilinganisha na majengo na miundombinu iliyojengwa. Hapa ndipo unaona Value for money,” amesema Mheshimiwa Joseph Kakunda, Mbunge wa Sikonge na Mjumbe wa PAC.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa chuo hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema mradi huo wenye majengo 17 umetekelezwa na VETA kupitia chuo cha VETA Singida na ofisi ya VETA Kanda ya Kati katika hatua tofauti tofauti na kwamba utekelezaji wake umefikia asilimia 99.4.
“Majengo yote yamefikia asilimia 100 ya ujenzi, kazi iliyobaki ni kuunganisha umeme (tail wire) kwa kila jengo kutoka kwenye nguzo za umeme zilizosambaza umeme katika eneo la chuo pamoja na kazi za nje,” amesema.
Amefafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo umegharimu kiasi cha Shilingi 3,004,013,405.56, ambapo fedha za ujenzi ni shilingi 2,653,915,038.00 na utengenezaji wa samani ni shilingi 350,098,367.56.