The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Prof. Mchome ahimiza fikra za kijasiriamali kukuza uzalishaji kwenye vyuo vya VETA
Posted on: Wednesday, 14 May 2025
Prof. Mchome ahimiza fikra za kijasiriamali kukuza uzalishaji kwenye vyuo vya VETA
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board), Prof. Sifuni Mchome, amehamasisha uongozi na wafanyakazi wa VETA kuelekeza nguvu zaidi katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazohitajika katika soko hapa nchini.
Prof. Mchome ameyasema hayo tarehe 8 Mei, 2025, wakati wa ziara ya Bodi hiyo katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Dar es salaam kujionea shughuli mbalimbali za utoaji mafunzo katika chuo hicho.
Prof. Mchome amesema ni wakati wa VETA kuhama kutoka kwenye mfumo wa kufundisha zaidi na kwenda kwenye mfumo wa kufundisha,kutenda na kuzalisha bidhaa, hali ambayo itaiwezesha VETA kujitegemea katika mambo mbalimbali .
“Tunataka tuone ni kwa namna gani VETA katika ukubwa wake inaweza kuzalisha bidhaa mbalimbali na kuziingiza sokoni kwa ajili ya matumizi,” amesema
Amesema VETA ina rasilimali yenye ujuzi pamoja na mitambo ya kisasa na kwamba kinachohitajika ni kujipanga kuwa wabunifu zaidi kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuweka mikakati ya kuzifikisha bidhaa hizo kwenye soko la ndani na nje ya nchi.