The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Ujerumani yaipatia VETA Sh. 650 milioni kuendeleza mafunzo ya Uanagenzi kwenye teknolojia ya Kilimo
Posted on: Monday, 01 November 2021
Taasisi ya Kijerumani ya “West German Skills Craft (WHKT) imetoa Euro 242,750 sawa na Shilingi za Kitanzania milioni 650 kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kuendeleza Mradi wa Mafunzo ya Uanagenzi Pacha kwenye teknolojia ya kilimo.
Randama ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya Mradi huo kwa awamu ya pili ilisainiwa Kati ya WHKT na VETA, Jumatatu, tarehe 25 Oktoba 2021 jijini Arusha na kuainisha mafunzo yatakayotolewa kwenye awamu hiyo kuwa ni Ufundi wa Zana za Kilimo na Teknolojia za udhibiti wa upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Akizungumza wakati wa warsha ya kuandaa mpango wa utekelezaji iliyofanyika sambamba na utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, ameishukuru WHKT kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa Mradi wa Mafunzo ya Uanagenzi kwenye sekta ya kilimo.
Alisema VETA na WHKT zimeshirikiana kwenye Mradi wa Uanagenzi Pacha tangu Aprili, 2017 kwa fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo kupitia chuo cha VETA Manyara ambapo jumla ya wanagenzi 72 (67 wanaume na 5 wanawake) walidahiliwa na wanatarajia kufanya mitihani yao ya kuhitimu mwezi Desemba 2021.
“Utekelezaji wa mradi huu kwa awamu ya kwanza kwenye fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Idadi ya makumpuni yanayoshiriki kwenye mpango huu yameongezeka kutoka mawili wakati mpango huu umeanza hadi 10 kwa sasa,” alisema.
Kwa mujibu wa Dkt. Bujulu, awamu ya pili ya mpango huo ilianza kutekelezwa mwezi Aprili, 2020 na itamalizika mwezi Machi, 2023 na utajikita kwenye uanzishwaji na upanuzi wa dhana ya mafunzo ya uanagenzi kwenye vyuo vingine zaidi vya VETA.
Alifafanua umuhimu wa mafunzo ya uanagenzi kwenye kuzalisha mafundi stadi bora akisema kwamba mfumo huo unaweka msingi imara wa kuimarisha uhusiano kati ya Taasisi za Mafunzo na Viwanda na hivyo kutoa mafunzo ya ufundi stadi yanayoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Naye Mtendaji Mkuu wa WHKT, Ndg. Matthius Heidmeier, alisema VETA na WHKT wanalenga kutoa ujuzi wa utendaji kazi kwa vijana ili kuwawezesha kuendesha maisha yao na kuchangia uchumi wa Taifa.
“Sisi WHKT tuna kauli mbiu inayosema “Tunajua Tunachokifanya.” Tunaamini kuwa kujifunza fani siyo tu mchakato wa utambuzi.Unajifunza vizuri zaidi ukitumia akili yako na milango yote ya fahamu. Hii ndiyo sababu elimu ya ufundi stadi ina umuhimu mkubwa sana nchini Ujerumani na Serikali ya Ujerumani imeweka juhudi kubwa kwenye mafunzo ya ufundi stadi kwa njia ya uanagenzi,” alisisitiza.
Alisema umuhimu wa mafundi stadi unaendelea kudhihirika katikati ya changamoto za dunia ikiwemo maendeleo ya kidigitali na mabadiliko ya tabia nchi akitoa mfano wa uhitaji mkubwa wa mafundi stadi kutokana na mafuriko yaliyoyakumba baadhi ya maeneo nchini Ujerumani.
“Ni miezi mitatu tu iliyopita ambapo tulipatwa na mafuriko makubwa yaliyoharibu maeneo mengi kwenye eneo la North Rhine – Westphalia na kusababisha miji, vijiji na watu kupoteza kila kitu walichokuwa nacho. Sasa maeneo hayo yanapaswa kujengwa upya na hivyo mafundi stadi wanahitajika kwa wingi," alisema.
Mfumo wa utoaji mafunzo ya Uanagenzi unahusisha kuhudhuria mafunzo chuoni na kufanya vitendo katika viwanda na mashamba au sehemu nyingine ya kazi. Mafunzo hayo ni ya miaka mitatu ambapo kwa mwaka mwanagenzi anatumia wiki 20 kwa mafunzo ya darasani na wiki 32 kwa mafunzo ya viwandani.
Mfumo huu una historia ndefu nchini Tanzania ambapo kwa miaka sita sasa (2011 hadi 2017) ulifanyiwa majaribio na VETA katika vyuo vyake vya Mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro. Chuo cha VETA Dar es Salaam kilifanya majaribio kwenye fani ya Umeme na Ufundi wa Magari huku Chuo cha VETA Moshi kikifanya majaribio kwenye fani ya Utalii na Ukarimu. Mafanikio hayo ndiyo yalipelekea kuanzishwa kwa mpango huu kwenye vyuo vingine vya VETA ambavyo ni VETA Manyara (Ufundi wa Zana za Kilimo), VETA Mbeya (Ufundi Bomba) na Mtwara (Ukarimu).
Awamu ya pili ya Mpango huu itajikita kwenye Teknolojia ya Kilimo na mafunzo yatatolewa kwenye vyuo vya VETA Kihonda, Arusha, Dakawa na Mpanda.