The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA, FIX CHAP KUFUNDISHA VIJANA 300 UJUZI WA KUREKEBISHA VIFAA VYA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Posted on: Friday, 11 July 2025
VETA, FIX CHAP KUFUNDISHA VIJANA 300 UJUZI WA KUREKEBISHA VIFAA VYA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Menejimenti ya VETA na uongozi wa Kampuni ya Fix Chap Limited ya jijini Dar es salaam wamekutana kujadili namna ya kushirikiana katika utoaji mafunzo kwa vijana watakaosaidia kwenye kurekebisha na kuunda vifaa vya umeme vitakavyotumika kupikia ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kikao kazi hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ndogo ya VETA Makao Makuu, jijini Dar es salaam, tarehe 9 Julai, 2025 kililenga kujadili namna ya kushirikiana katika kuzalisha mafundi watakaorekebisha zana zinazotumia nishati ya umeme kupikia kama Pressure cooker, Rice Cooker, Air frier na Induction cooker ambavyo kwa sasa havina wataalamu wa kutosha kuvirekebisha pindi vinapoharibika.
Takriban vijana 300 wanatarajiwa kufikiwa na kupewa mafunzo ya urekebishaji vifaa vya kupikia vya umeme kupitia kampuni ya Fix chap katika mikoa 6 ya Dar es salaam, Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya na Zanzibar kama sehemu ya kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kampeni ya matumizi ya nishati safi na jadidifu na utunzaji wa mazingira.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Prince Tillya amesema, kampuni yake imeona fursa katika eneo hilo.
Amesema vifaa vingi vinavyotumia umeme kupikia havitumiki sana kwa kuwa havipatikani kwa wingi lakini pia hakuna nguvukazi yenye ujuzi wa kuvirekebisha mara vinapoharibika na kuona ni wakati sasa wa kuwazalisha wataalamu hao kupitia mashirikiano na VETA.
Naye Mkurugenzi Mkuu, CPA Antony Kasore amesema VETA ipo tayari kushirikiana na kampuni hiyo katika eneo la kusajili kozi fupi zitakazowaandaa vijana wengi zaidi katika eneo hilo.
Amesema, VETA itaipitia mitaala ya umeme na elektroniki ilu kuona kama inakidhi uhitaji wa kozi fupi wanazohitaji katika utekelezaji wa Mafunzo hayo pamoja na kuwajengea uwezo walimu katika vyuo vya VETA nchini ili waweze kutumika kutoa mafunzo hayo.
“Jukumu letu kama VETA ni kuona mahitaji ya soko la ajira nchini yanatimizwa na kufikiwa katika kuhakikisha kuwa tunaandaa kundi kubwa la vijana watakaowasaidia Watanzania wanaotumia vifaa hivyo kuwa salama na ikiwezekana bidhaa hizi kuundwa na kuzalishwa hapa nchini. Hivyo kushirikiana pamoja nanyi tutasaidia kuokoa kundi kubwa la vijana wasio na ajira na kuwafikia Watanzania wengi zaidi wenye uhitaji katika eneo hilo,” amesisitiza CPA Kasore