The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA kushirikiana na makampuni ya Mradi wa Ujenzi Bomba la Mafuta (EACOP) kutoa mafunzo kwa vijana
Posted on: Friday, 17 February 2023
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na Makampuni ya Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi – East Africa Crude Oil Pipeline (EACOP) wanatarajia kutoa mafunzo kwa vijana 170 nchini wanaoshiriki kwenye mradi huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo tarehe 15 Februari, 2023 katika chuo cha VETA Tanga, Kamishna wa Mafuta na Gesi kutoka Wizara ya Nishati, Ndugu Michael Mjinja amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa wafanyakazi 170 wanaotekeleza shughuli mbalimbali kwenye mradi wa bomba la mafuta ambao wataboreshewa ujuzi wao ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mradi.
Ndugu Mjinja amesema mafunzo hayo yanatolewa na kampuni ya Daqing Oilfield Construction Group Co.Ltd (DOCG) kupitia kampuni ya Kimataifa ya Sunmaker Development and Consulting (TZ) Ltd ambapo wahitimu wa mafunzo hayo watapatiwa vyeti vinavyotambulika kimataifa vitakavyowawezesha kufanya kazi popote duniani.
Amesema washiriki wa mafunzo hayo watapata utaalamu wa ufundi kwenye miradi inayohusiana na sekta ya mafuta na gesi na kuweza kutumia utaalamu huo kwenye mradi wa bomba la mafuta na miradi mingine nchini ili kukuza maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi nchini Tanzania.
Walimu wa fani mbalimbali katika chuo cha VETA cha Mkoa wa Tanga wanatarajia kunufaika na mafunzo hayo yatakayotolewa chuoni hapo.
Miongoni mwa utaalamu utakaotolewa kupitia mafunzo hayo ni wa ukaguzi wa afya, usalama na mazingira, uendeshaji wa mashine ardhini, uendeshaji wa mitambo pamoja na ufundi wa umeme na vifaa mbalimbali.
Mwanasheria wa VETA, Wakili Dora Mweta aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA kwenye hafla hiyo amesema kuwa VETA inasikia fahari kushiriki kwenye mradi huo wenye manufaa makubwa kwa Taifa ambao pia unatoa fursa nyingi za ajira kwa vijana.
Amesema mafunzo yakayotolewa katika chuo cha VETA Tanga ambayo walimu wa VETA watashiriki, yatawaongezea ujuzi walimu hao na kuwapa uzoefu kwenye eneo la mafuta na gesi na hatimaye walimu hao kuwafundisha wanafunzi katika chuo hicho.
Wakili Mweta alitoa rai kwa makampuni na wadau mbalimbali kuiunga mkono Serikali katika kuwasomesha vijana na kuwawezesha kupata ajira.
Uzinduzi wa mafunzo hayo umehusisha Wizara ya Nishati, Serikali ya Mkoa wa Tanga na watendaji wa mashirika ya TPDC, EWURA, VETA na Chuo cha Ufundi Arusha ambapo washiriki wa hafla hiyo walipata fursa ya kutembelea eneo lilipowekwa jiwe la msingi la mradi huo na maeneo yatakapowekwa matanki ya mafuta.
Ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima - Magharibi mwa Uganda mpaka kwenye bandari ya bahari ya Hindi, Tanga wenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,443 zikiwemo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania unatarajia kuzalisha ajira zipatazo 10,000.