The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA KUSHIRIKIANA NA YUNIVESO KUWAWEZESHA VIJANA KUJIAJIRI
Posted on: Friday, 16 August 2024
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ipo mbioni kuanzisha ushirikiano na taasisi ya Yuniveso katika kuhakikisha wahitimu wa ufundi stadi wanajengewa uwezo wa kujiajiri kupitia vituo vya uatamizi na ubunifu.
Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Yuniveso Consultancy na Menejimenti ya VETA, kwenye Ofisi za VETA Makao Makuu, jijini Dodoma, tarehe 14 Agosti 2024, Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Bi Fatma Mshinda amesema mpango huo unalenga kuimarisha umahiri kwa wahitimu, kuwaunganisha vijana wenye ujuzi unaofanana na kuwa kitu kimoja ili kuleta ufanisi badala ya kushindana wao kwa wao.
Amesema wahitimu pia watawezeshwa kushiriki katika matamasha mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ili kuweza kutangaza kazi na bidhaa zao.
“Sisi hatuna utaalam wa kutoa mafunzo, hivyo kazi ya kutoa mafunzo itabaki kwa VETA na sisi tutawawezesha wahitimu kutoka VETA katika ajira na fursa mbalimbali,” amefafanua.
Mkurugenzi Mkuu, CPA Anthony Kasore, amesema VETA imepokea kwa mikono miwili mpango huo kwa kuwa unaenda sambamba na malengo yake ya kuwawezesha vijana kuwa wabunifu, kuajiriwa na kujiajiri kupitia ufundi stadi.
CPA Kasore ameelekeza kuundwa kwa timu inayohusisha pande zote mbili ili kuandaa andiko mahsusi kwa ajili ya utekelezaji wa ushirikiano huo.