The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA, UJUMBE KUTOKA INDIA WAJADILI USHIRIKIANO KATIKA MAFUNZO YA TEHAMA
Posted on: Friday, 11 July 2025
VETA, UJUMBE KUTOKA INDIA WAJADILI USHIRIKIANO KATIKA MAFUNZO YA TEHAMA
Menejimenti ya VETA Makao Makuu, Kanda ya Dar es salaam na Chuo cha VETA cha mkoa wa Dar es salaam wamekutana leo tarehe 9 Julai, 2025 na wawekezaji, wafanyabiashara na maafisa wa serikali kutoka jimbo la Haryana la nchini India kwa lengo la kujadili namna bora ya kushirikiana katika eneo la utoaji Mafunzo ya TEHAMA.
Kiongozi wa msafara wa wawekezaji hao, Ndg. Mukesh Bajaj amesema kikao kazi hicho ni sehemu ya kufungua milango ya ushirikiano kati yao na VETA katika maeneo mbalimbali yakiwemo habari, usalama wa mtandao, akili mnemba, uchambuzi wa taarifa, mitandao na matumizi ya simu pamoja na uzuiaji uhalifu wa kimtandao.
"Kupitia kampuni yetu ya Haryana State Electronics Development Coorperation Limited yenye vituo 100 vya mafunzo ya dijitali vilivyoidhinishwa mjini na vijijini kwenye maeneo mbalimbali duniani hatutahakikisha tu kwamba tumezalisha vijana wenye ujuzi stahiki katika soko la ajira bali tutashirikiana pia kutoa mtaala rahisi na unaoweza kubadilika kulingana na mabadiliko ya teknolojia tunayoongelea leo," amesisitiza ndugu Bajaj.
Akiwakaribisha wawekezeaji, wafanyabiashara na maafisa hao kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Mkurugenzi wa VETA, Kanda ya Dar es salaam, Ndg.Wilhard Soko ameomba kuwa pamoja na kutoa mafunzo kwa wanafunzi kupitia vyuo mbalimbali vya VETA, ushirikiano huo pia usaidie kuwaandaa walimu pamoja na kuwajengea uwezo watumishi mbalimbali ili kuwarahisishia kwenye kutoaji mafunzo stahiki kwa wanafunzi.
Pamoja na kikao kazi hicho wawekezaji hao wamepata fursa ya kutembelea karakana za Umeme, Elektroniki, Mitambo, Uchapaji kwa lengo la kujionea namna mafunzo yanavyotolewa katika karakana hizo.