The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA YAAGIZWA KUONGEZA UZALISHAJI KWENYE BIDHAA NA BUNIFU ZAKE
Posted on: Wednesday, 20 August 2025
VETA YAAGIZWA KUONGEZA UZALISHAJI KWENYE BIDHAA NA BUNIFU ZAKE
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imeagizwa kuongeza uzalishaji zaidi katika bidhaa, vifaa na bunifu zinazozalishwa na wanafunzi, wahitimu na walimu wake, ili kuweza kutatua changamoto za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi zinazowakabili Watanzania wengi.
Rai hiyo imetolewa tarehe 7 Julai, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board), Prof. Sifuni Mchome, alipotembelea banda la VETA katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo (Nanenane), Nzuguni, jijini Dodoma na kujionea namna VETA inavyotumia Maonesho hayo kutangaza bidhaa, vifaa, bunifu zinazotengenezwa kwenye vyuo vyake kote nchini pamoja na fursa mbalimbali za mafunzo ya muda mrefu na mfupi.
Prof.Sifuni amesema, Tanzania ina zaidi ya watu milioni 60 ambapo nusu yao wanajishughulisha na Kilimo, Ufugaji na Uvuvi na wanahitaji bidhaa na huduma tunazozalisha katika vyuo vyetu ili kurahisisha na kuongeza tija katika shughuli zao.
"Nendeni mkazalishe kwa wingi, tuongeze vipato na wataalamu watakaokwenda popote kuwasaidia Watanzania kama sehemu ya maono ya Bodi yetu yanayohimiza kutoka kwenye utoaji wa mafunzo na kwenda kwenye uzalishaji," amesisitiza Mchome.
Aidha, Mchome amesisitiza ushirikiano baina ya VETA na wadau wengine wa maendeleo wanaotegemea bidhaa za VETA kuweza kuzalisha na kuwafikia Watanzania wengi zaidi.