Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea kung’ara katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (maarufu kama Sabasaba) ambapo licha ya kuvutia watu wengi kutembelea banda lake, VETA imeibuka mshindi wa tatu katika kundi la Elimu, Utafiti na Uendelezaji Ujuzi kwenye maonesho hayo ya 44 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 1 hadi 13 Julai 2020.
Katika Maonesho hayo, VETA ilionesha fursa za mafunzo ya ufundi stadi, bidhaa, ubunifu pamoja na teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na walimu, wanafunzi na wahitimu wake ili kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.
Mshindi wa kwanza kwenye kundi la Elimu, Utafiti na Uendelezaji Ujuzi ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nafasi ya pili ilichukuliwa na Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).
Baadhi ya ubunifu uliokuwa kivutio zaidi kwa watembeleaji wa maonesho hayo ni mashine ya kuzidua Unga wa Ubuyu inayoendeshwa kwa umeme, Mfumo wa kielektoniki unaowezesha umeme kuingizwa kwenye mita za umeme baada ya kulipia kwa njia ya simu, Meza ya kupasha moto Chakula na Kupoza Vinywaji, Mtambo wa kuchemsha maji pasipo kutumia umeme, kochi linaloweza kubadilika kuwa kitanda, vifaa vya umwagiliaji na kifaa cha kurahisisha kupanda mbegu shambani.
VETA pia ilionesha namna ilivyochangia katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, (COVID 19 kwa kutengeneza vitakasa mikono, sabuni za maji, mashine za kunawia mikono na barakoa.
Katika maonesho hayo, VETA ilitembelewa na jumla ya wananchi 7,448, wakiwemo viongozi wa kitaifa wengi wao walifurahishwa na kupongeza juhudi zinazofanywa na VETA hasa katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana nchini huku wakishauri kutanua wigo wa utoaji mafunzo ya ufundi stadi ili kufikia makundi mengi zaidi.
Miongoni mwawageni waliotembelea Banda la VETA ni Katibu wa Bunge Ndg. Stephen Kagaigai ambaye alisifia VETA kwa kuwa na teknolojia nzuri za ubunifu wa hali ya juu na kuishauri VETA kuwaimarisha zaidi vijana wanaopata mafunzo katika vyuo hivyo ili waweze kushindana katika soko.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa ushindi huo umetoa hamasa kwa VETA kuendelea kuboresha zaidi utoaji mafunzo ya ufundi stadi na kuendeleza ubunifu na teknolojia mbalimbali ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda nchini.
Maonesho hayo yaliyoongozwa na kauli mbiu, “Maendeleo ya Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu (Industrialization for Job Creation and Sustainable Development), yalifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, tarehe 2 Julai 2020, na kufungwa na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Balozi Amina Salum Ali.
Maonesho hayo yalihudhuriwa na Makampuni, Taasisi na Mashirika yapatayo 2,880 ya ndani na nje ya nchi.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office