Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeibuka Mshindi wa Kwanza katika kundi la Elimu, Utafiti na Uendelezaji Ujuzi na Mshindi wa Tatu wa Jumla katika maonesho ya 43 ya Biashara Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika viwanja vya Mwalimu J.K Nyerere jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi Jumanne, tarehe 2 Julai 2019 na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia alitunuku vikombe kwa washindi wa kwanza wa makundi mbalimbali na washindi wote wa jumla.
Katika kundi la Elimu, Utafiti na Uendelezaji Ujuzi VETA ilifuatiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichoshika nafasi ya pili na Taasisi ya Uhasibu (TIA) iliyoshika nafasi ya tatu.
Maonesho hayo yameshirikisha makampuni, taasisi na mashirika ya ndani 3,250 ambapo washindi wa jumla walikuwa ni Jeshi la Magereza lililoshika nafasi ya Kwanza, Jeshi la Kujenga Taifa nafasi ya pili na VETA nafasi ya Tatu.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo za ushindi huo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa tuzo hizo zinatoa hamasa ya kufanya kazi kwa kujituma pamoja na kuendelea kubuni vitu mbalimbali kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Amesema VETA pia inatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa vyuo ili kuwafikia watanzania wengi katika utoaji mafunzo na uendelezaji ujuzi kwa maendeleo ya viwanda na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba) yalianza tarehe 28 Juni 2019 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 13 Julai 2019 na yana Kauli mbiu ya “Usindikaji wa Mazao ya Kilimo kwa Maendeleo Endelevu ya Viwanda.” Nchi 35 zinashiriki katika maonesho hayo.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office