The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA yasaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha World Peace cha Cyprus ya Kaskazini
Posted on: Wednesday, 18 June 2025
VETA yasaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha World Peace cha Cyprus ya Kaskazini
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha World Peace (WPU) kilichopo Jamhuri ya Cyprus, Kaskazini mwa Uturuki, ikiwa ni hatua muhimu ya kuendeleza na kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo, tarehe 18 Juni 2025, kwenye Chuo cha WPU, Jamhuri ya Cyprus, kati ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore na Mkuu wa Chuo Kikuu cha World Peace, Profesa Behiye Cavusoglu, ambapo pande hizo mbili zimekubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya elimu na mafunzo.
Miongoni mwa maeneo ya ushirikiano yaliyoainishwa katika makubaliano hayo ni pamoja na kubadilishana uzoefu na ujuzi kati ya walimu na wanafunzi wa pande zote mbili, kutekeleza programu za pamoja za mafunzo na utafiti, pamoja na kuanzisha miradi ya pamoja ya kiufundi na kitaaluma.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, CPA Anthony Kasore amesema VETA itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za kitaaluma na wadau wa maendeleo ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuinua viwango vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
“Ushirikiano huu na Chuo Kikuu cha World Peace ni ushahidi kuwa VETA imejizatiti katika kuhakikisha inawapatia wanafunzi na walimu wake fursa za kimataifa ili kuongeza maarifa, ubunifu na ushindani wa kitaifa na kimataifa katika eneo la ufundi stadi,” amesema CPA Kasore.
Kwa upande wake, Prof. Behiye Cavusoglu alieleza kufurahishwa na hatua hiyo, akibainisha kuwa Chuo cha World Peace kiko tayari kushirikiana na VETA katika kuhakikisha mafanikio ya makubaliano hayo yanaonekana kwa vitendo kwa manufaa ya wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Makubaliano haya yanatarajiwa kufungua milango zaidi ya ushirikiano wa kimataifa kwa VETA na kuchochea maendeleo ya sekta ya elimu ya ufundi nchini Tanzania.