Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imewajengea uwezo watahini 256 kwa ajili ya kuendesha awamu ya pili ya zoezi la kurasimisha ujuzi kwa mafundi 10,443 nchini.
Akizungumza wakati wa kufunga semina kwa watahini hao kwenye chuo cha VETA Singida Julai 17, 2019, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Anthony Kasore alisema kuwa semina hiyo ililenga kutoa mfunzo ya kuwawezesha watahini hao kuendesha zoezi la tathmini kwa ufanisi.
Semina hiyo iliyojumuisha watahini kutoka katika vyuo vya Ufundi Stadi na kutoka viwanda mbalimbali ilifanyika katika chuo cha VETA Singida tarehe 8 hadi 17 Julai 2019.
Kasore aliwataka watahini kufuata miongozo na maelekezo waliyopewa juu ya uendeshaji wa zoezi hilo na kuwataka kutanguliza uzalendo na uadilifu katika hatua zote za utekelezaji wa kazi hiyo.
“Nawaomba sana mzingatie taratibu zote zinazotakiwa katika utekelezaji wa zoezi hili,” alisema
Kwa mujibu wa Kasore, zoezi hilo la tathmini linatarajiwa kuanza Julai 30, 2019 nchi nzima ambapo mafundi waliopata ujuzi kupitia mfumo usio rasmi watafanyiwa tathmini kulingana na ujuzi walionao kisha kupewa mafunzo kuziba mapungufu na hatimaye kutunukiwa vyeti ambavyo vitawawezesha kutambulika na kukubalika katika mfumo rasmi wa ajira.
Naye Mratibu wa programu hiyo kutoka VETA, Bwire Ally alisema kuwa katika mafunzo hayo watahini hao walifundishwa namna ya kutambua, kukusanya takwimu na kufanya tathmini ya ujuzi kwa mafundi.
Bwire alisema kukamilika kwa mafunzo hayo kumeongeza idadi ya watahini kutoka 344 hadi 600 ambao watafanya tathmini katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema miongoni mwa faida za programu hiyo ni kuwasaidia mafundi waliojifunza kupitia sehemu za kazi (wanagenzi) kupata kazi zenye staha; kuwawezesha kushiriki na kushindana kikamilifu katika soko la ajira; pamoja na kuinua tija mahali pa kazi na kusaidia waajiri wenye makampuni kukidhi viwango katika eneo la rasilimali watu.
Mmoja wa watahini waliopatiwa mafunzo hayo kutoka chuo cha VETA Iringa Gereon Mmole alisema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea mwanga zaidi na uelewa juu kuendesha zoezi la tathmini kwa mafundi.
Zoezi la utambuzi na urasimishaji wa ujuzi (Recognition of Prior Learning – RPL) linaloendeshwa na VETA kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu lilianza Julai 3, 2017 ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya vijana 3,989 wanaume 3,539 na wanawake 450 walirasimishwa ujuzi wao.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office