The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA YAWAKUTANISHA WADAU KUBORESHA MITAALA SEKTA YA UTALII
Posted on: Monday, 22 September 2025
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imewakutanisha wadau wa sekta ya utalii nchini kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni ya uboreshaji wa mitaala ya kozi za Uongozaji Watalii na Uendeshaji wa Usafiri na Utalii kwa ngazi ya Stashahada.
Kikao hicho kilifanyika tarehe 20 Septemba 2025 katika Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii, jijini Arusha, kikilenga kuhakikisha mitaala hiyo kuwa shirikishi na kuendana na mabadiliko ya sekta ya utalii.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kupitia majadiliano hayo, wadau wataweza kubaini mapungufu ya mitaala iliyopo, kupendekeza maeneo mapya na kutathmini namna mitaala hiyo inavyoweza kuchangia katika ajira endelevu na huduma bora katika sekta ya utalii.
Alipongeza juhudi za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa sekta ya utalii kipaumbele kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo filamu ya The Royal Tour iliyoasisiwa na Rais, hatua iliyoongeza hamasa na mahitaji ya wataalamu katika sekta hiyo.
“Ni muhimu kuwa na mitaala inayozalisha wataalamu wenye weledi watakaoweza kuajiriwa, kujiajiri na kuliingizia Taifa mapato kupitia sekta hii yenye fursa kubwa,” amesema CPA Kasore.
Aidha, CPA Kasore amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya vyuo na waajiri ili kuzalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira, akisisitiza kuwa wahitimu wanapaswa kuwa tayari kwa kazi bila kuhitaji mafunzo ya muda mrefu kazini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, VETA, Dkt. Abdallah Ngodu, amesema ushirikishaji wa wadau ni hatua muhimu ya kuhakikisha mitaala inalingana na mazingira halisi ya kazi na matarajio ya waajiri.
Akizungumza kwa niaba ya wadau, Bi. Kowena Malijani kutoka kampuni ya Garireli Link Travel Company, amesema waajiri hukutana na changamoto hasa katika eneo la lugha na huduma kwa wateja, na kwamba maoni yao yamewasilishwa ili yafanyiwe kazi.
Ametoa wito kwa vijana kuchangamkia kozi za sekta ya utalii akisema ni sekta inayokua kwa kasi na yenye fursa nyingi za ajira.