The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Vijana 1000 kunufaika na mafunzo ya ufundi zana za kilimo kupitia ushirikiano wa VETA na AGRICOM
Posted on: Friday, 12 May 2023
Vijana elfu moja (1000) nchini wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya Ufundi wa Zana za Kilimo, kupitia ushirikiano kati ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Kampuni ya Agricom.
Hayo yamebainishwa tarehe 10 Mei, 2023, baada ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Agricom kuweka saini za makubaliano ya ushirikiano wa kutoa mafunzo ya Ufundi wa Zana za Kilimo.
Kupitia ushirikiano huo, Kampuni ya Agricom ambayo inajishughulisha na kilimo na uuzaji wa vipuri na zana za kilimo, itawezesha kuboresha utoaji mafunzo ya ufundi wa Zana za Kilimo kwa walimu na wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo zaidi na kupata uzoefu kwenye mazingira halisi ya kazi.
Akizungumza baada ya kuweka saini ya makubaliano ya ushirikiano, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema VETA itashirikiana na Agricom.
kutoa mafunzo kwa mfumo wa Uanagenzi Pacha na kuandaa wakufunzi wabobezi (Master Trainers) ambao watatumika kuboresha umahiri wa wanafunzi kwenye fani za uungaji vyuma, ufundi magari pamoja na ufundi wa mitambo na zana za kilimo na hatimaye kuzalisha wahitimu wanaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
CPA Kasore alivitaja vyuo vya VETA vitakavyohusika na utoaji mafunzo kwenye mradi huo kuwa ni Dakawa, Kihonda, Arusha (Oljoro), Manyara na Mpanda.
CPA Kasore alisema VETA itaendelea kuboresha utoaji mafunzo kwenye sekta ya kilimo ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita za kuwezesha vijana kushiriki kwenye kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Agricom Ndg. Alex Duffar, alisema ushirikiano huo utawezesha upatikanaji wa mafundi mahiri, wenye uzoefu watakaoweza kufanya ukarabati wa zana mbalimbali za kilimo na kuanzisha biashara zao.
Alisema vijana watakaohitimu mafunzo wataweza kufanya matengenezo kwenye vifaa na mitambo mbalimbali ya kilimo ikiwemo Matrekta, ‘Powertillers’, ‘Combine Harvesters’, mashine za kukaushia mazao na zana nyingine za kilimo.