The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VIJANA 200 KUNUFAIKA NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI KUPITIA MPANGO WA ‘SEED’
Posted on: Friday, 11 July 2025
VIJANA 200 KUNUFAIKA NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI KUPITIA MPANGO WA ‘SEED’
Jumla ya vijana 200 kutoka vyuo vya VETA Dar es Salaam, Kipawa ICT Centre na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni (FDC) wanatarajia kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi kupitia Mpango wa Ujuzi kwa Maendeleo ya Ujasiriamali na Ajira (SEED) unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya NMB, NMB Foundation na Shirika la Save the Children.
Akizindua mpango huo tarehe 9 Julai,2025, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema mpango wa SEED unaunga mkono jitihada za Serikali za kuongeza fursa za ajira na kukuza ujuzi wa vijana nchini Tanzania.
Prof. Mkenda amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wadau katika kukuza fursa za ajira kwa vijana na itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha vijana wanapata ujuzi wa kisasa unaokidhi mahitaji ya soko.
“Tunataka kuona bidhaa bora zinazozalishwa hapa nchini zikitokana na vijana waliopitia VETA. Lengo letu ni kuandaa vijana wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya soko, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa,” amesema
Aidha, Waziri Mkenda amebainisha kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa vyuo 65 vya VETA nchini kote, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na chuo cha ufundi stadi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa NMB, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Foundation, Bi. Ruth Zaipuna, amesema SEED inalenga kuwapa vijana mafunzo ya kuanzisha na kusimamia biashara endelevu kwa mafanikio na kupunguza tatizo la ajira nchini.
Zaipuna ameongeza kuwa programu hiyo inalenga kuwa endelevu na kuwafikia vijana zaidi kutoka mikoa mingine.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Mzee Kasore, amesema kuwa mafunzo hayo ya ufundi stadi yatawawezesha vijana kujiajiri, kuajiriwa au hata kuwaajiri wenzao.
“Mradi huu unakwenda sambamba na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha kila kijana anapata ujuzi utakao msaidia kuishi maisha bora. SEED ni mfano wa ushirikiano wenye matokeo chanya kwa Taifa letu,” amesema.