Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi imeendelea kusogeza zaidi huduma za mafunzo kwa wananchi kupitia ujenzi wa vyuo vipya katika ngazi ya wilaya na halmashauri.
Juhudi hizo zimeendelea kujidhihirisha kwa vyuo katika wilaya mbalimbali kukamilika na kuzinduliwa rasmi miongoni mwake ikiwa ni Chuo cha VETA Nyamidaho (wilayani Kasulu), VETA Nkasi na VETA Ileje.
VETA iliuaga mwezi Juni na kuukaribisha mwezi Julai kwa uzinduzi wa vyuo vipya katika wilaya za Kasulu, Nkasi na Ileje ambapo Chuo cha Ufundi Stadi Nyamidaho (VETA Nyamidaho) wilayani Kasulu kilizinduliwa tarehe 29 Juni, 2020, Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Nkasi (VETA Nkasi) tarehe 2 Julai, 2020 na Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ileje (VETA Ileje) tarehe 3 Julai, 2020.
Vyuo hivyo vilizinduliwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ambaye alieleza kuwa ukamilishaji wa vyuo hivyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga vyuo vya ufundi stadi katika kila Wilaya nchini ili kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanafika karibu zaidi na wananchi.
Alisema katika mwaka wa fedha 2019/20, Serikali ilikamilika ujenzi wa vyuo 10 katika Wilaya za Namtumbo, Urambo, Ndolage, Nkasi, Ileje, Kanadi, Chato, Samunge, Gorowa na Mabalanga.
Waziri Ndalichako aliwataka wananchi wa Wilaya za Kasulu, Nkasi na Ileje kutumia vyuo hivyo kujipatia ujuzi ili kuweza kushiriki kikamilifu kuijenga Tanzania ya viwanda hasa kwa kujiajiri kwa kufungua viwanda vidogo vidogo katika Wilaya zao na kuajiri watu wengine.
“Mafunzo ya ufundi stadi ni mkombozi mkubwa katika kukabiliana na tatizo la ajira, kwani ujuzi wa ufundi stadi unampa mhitimu fursa ya kuajiriwa na kujiajiri,” alisema.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika uzinduzi wa vyuo hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema uwezo wa kudahili wanafunzi wa kozi za muda mrefu wa VETA Nyamidaho ni 160, VETA Nkasi 160 na VETA Ileje 120, hivyo kwa pamoja vyuo hivyo vina uwezo wa kudahili jumla ya wanafunzi 440 kwa mafunzo ya muda mrefu, wakati kwa upande wa kozi za muda mfupi ni wanafunzi 1000.
Fani zitakazotolewa katika vyuo hivyo kwenye mabano ni VETA Nyamidaho (Uashi, Ushonaji, Uhazili na Matumizi ya Kompyuta, na Umeme wa Majumbani); VETA Nkasi (Ushonaji, Uhazili na Matumizi ya Kompyuta, Umeme wa Majumbani na Bidhaa za Ngozi) na VETA Ileje (Ushonaji, Uhazili na Matumizi ya Kompyuta, na Umeme wa Majumbani).
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Peter Maduki alishukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi na kuagiza uongozi wa VETA kutoa mafunzo ya muda mfupi ya fani ya Uashi bure kwa wananchi wanaohitaji mafunzo hayo katika kata ya Nyamidaho.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo alishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kukamilisha ujenzi wa chuo cha VETA Nkasi na kuwataka wananchi wa Nkasi kutumia vyema chuo hicho kujipatia ujuzi na kuleta maendeleo mkoani hapo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Bregedia Jenerali Nicodemus Mwangela alisema kuwa chuo cha VETA Ileje kitakuwa mkombozi mkubwa sana kwa vijana ambao wamekuwa wakihitaji mafunzo kwa ajili ya kujipatia ujuzi kwenye fani mbalimbali.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office