Mkurugenzi wa Ufundi, Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Noel Mbonde amewaasa wakufunzi na watumishi wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kuzingatia weledi katika kuandaa walimu bora wa ufundi stadi nchini.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa Mafunzo juu ya Misingi na Taratibu za Uendeshaji Utumishi wa Umma kwa watumishi wa Chuo hicho mjini Morogoro tarehe 16 Oktoba, 2020 Dkt Mbonde alisema kuwa MVTTC imebainishwa kuwa Chuo cha mfano cha kuandaa walimu wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na hivyo ni muhimu kuwa na Watumishi wenye uweledi katika kutekeleza majukumu yake.
“Naamini kabisa kuwa mafunzo mliyoyapata yataboresha kwa kiwango kikubwa utendaji wenu wa kazi na kufanya chuo hiki kutekeleza kwa weledi jukumu lake muhimu sana la kuandaa walimu wa ufundi stadi nchini… Kumbukeni kuwa jukumu mlilonalo ni kubwa sana kwa ustawi wa maendeleo ya nchi,” Alisema.
Mafunzo hayo ya siku tano yaliandaliwa kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kupitia Mradi wa Elimu Bora kwa Ukuaji wa Afrika Awamu ya Pili, (Better Education for Africa’s Rise-Phase Two-BEAR II).
Pamoja na masuala mengine Mradi huo unalenga kuongeza ubora wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET).
Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema kuwa VETA itaendelea kukiboresha chuo cha MVTTC kwa kurekebisha miundombinu mbalimbali, kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia, na kuwajengea uwezo watumishi wote ili wawe na weledi katika kutekeleza majukumu yao.
Dkt. Bujulu alishukuru UNESCO kwa ushirikiano mkubwa katika kufadhili afua mbalimbali za Elimu na Mafunzo ya ufundi Stadi na kukishukuru Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) kwa uwezeshaji wa mada mbalimbali kwa watumishi hao.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA Stella Ndimubenya alitaja mada mbalimbali zilizotolewa kuwa ni pamoja na Maadili ya Utumishi wa Umma, Menejimenti ya kumbukumbu za Serikali, Usiri na Uendeshaji wa Ofisi za Umma, Maboresho katika Utumishi wa Umma na Usimamizi wa Utendaji Kazi Serikalini pamoja na Upimaji wa Utendaji kwa uwazi (OPRAS). Nyingine ni Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 08 ya mwaka2002 na marekebisho yake, Huduma bora kwa Mteja, Uzingatiaji wa Muda, Kudhibiti Msongo wa Mawazo pamoja na maelekezo ya namna ya Kupambana na Rushwa Mahala pa Kazi.
Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) ni chuo pekee nchini kinachofundisha walimu wa ufundi stadi na kinamilikiwa na VETA.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office