The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
WALIMU 51 WA VYUO VYA VETA WAPATIWA ELIMU YA MBINU ZA UTOAJI MAFUNZO YA UFUNDI UMEME
Posted on: Friday, 11 July 2025
WALIMU 51 WA VYUO VYA VETA WAPATIWA ELIMU YA MBINU ZA UTOAJI MAFUNZO YA UFUNDI UMEME
Jumla ya walimu 51 wa fani ya Umeme kutoka vyuo vya VETA vya wilaya na mikoa kote nchini wamepatiwa Elimu ya namna ya ufundishaji wa Mafunzo hayo kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu mada mpya zilizoongezwa katika mtaala wa umeme.
Akifunga rasmi mafunzo hayo yaliyochukua muda wa siku 10, tarehe 1 Julai, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha VETA cha mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore amewataka walimu hao kwenda kutekeleza wajibu wao kwa kutumia elimu waliyoipata na rasilimali zinazopatikana katika vyuo vyao ili mafunzo watakayoyatoa yakawandae vijana kupata ujuzi utakaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Tunaona kwenye eneo la Umeme fursa zimebadilika na zipo fursa nyingi, katumieni fursa hii mliyoipata kwenda kushirikiana na walimu wengine waliopo huko ambao hawakupata nafasi ya kupata mafunzo haya kuhakikisha mafunzo yanatolewa kwa weledi na kuongeza uzalishaji, “ Kasore amesisitiza.
Naye mratibu wa Mafunzo hayo, Afisa Mkuza Mitaala kutoka VETA Makao Makuu ndugu Edwin Godwin amesema dhima kuu ya mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo walimu hao kwenda kutekeleza mtaala uliohuishwa wa mwaka 2022 ambapo yamejumuisha mafunzo ya mwalimu mmoja mmoja kwa nadharia na kwa vitendo.
Akimshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa niaba ya wengine, mwenyekiti wa walimu hao, Ndugu Selemani Mlangi kutoka chuo cha VETA-Dodoma amesema miongoni mafunzo waliyoyapata ni mafunzo ya mfumo wa umeme jua, programmable Logic Controller, usukwaji wa mota, fensi za umeme, CCTV na Transfomer rewinding huku akiahidi kwenda kuyatumia mafunzo hayo kuvisaidia vyuo vyao kufikia lengo la VETA la utoaji mafunzo yenye weledi wa watanzania wenye uhitaji.