The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
WASAJILI 78 WAPATIWA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA UTOAJI MAFUNZO YA UFUNDI STADI
Posted on: Friday, 11 July 2025
WASAJILI 78 WAPATIWA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA UTOAJI MAFUNZO YA UFUNDI STADI
Jumla ya wasajili 78 kutoka vyuo vya VETA vya mikoa na wilaya kote nchini wamepatiwa Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa mbinu bora za usimamizi wa utoaji Mafunzo ya Ufundi Stadi katika vyuo vyao kote nchini.
Mafunzo hayo ya siku moja, yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha VETA cha mkoa wa Dodoma tarehe 25 Juni, 2025.
Akifunga mafunzo hayo Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore amewataka Wasajili hao kwenda kutumia elimu na maarifa waliyoyapata kupitia Mafunzo hayo kutimiza jukumu la utoaji mafunzo ya Ufundi Stadi kwa viwango, ubora na kuzingatia mahitaji ya soko la ajira nchini.
“ Ili wananchi wa maeneo yanayotuzunguka waone na kufahamu umuhimu wetu kama VETA ni lazima tuhakikishe kwamba tunafahamu ujuzi wanaohitaji kupitia shughuli za kiuchumi na kijamii zinazofanyika katika maeneo yao na tuwape mafunzo yanayozingatia misingi na taratibu zinazotuongoza katika utoaji Mafunzo hayo ili tuweze kukidhi mahitaji ya wananchi hao,” amesema Kasore.
Pamoja na utoaji wa Mafunzo, Kasore amewaasa watumishi hao kwenda kuwa wabunifu katika matumizi sahihi ya nyenzo za mafunzo pamoja na kutumia mitaala mahsusi katika utoaji mafunzo hayo.
Naye Mdhibiti Ubora wa Mafunzo, kutoka VETA Makao Makuu, Bi. Gloriana Kakuru, ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha watumishi hao kuwa na uelewa mpana wa utaratibu wa udahili wa wanafunzi watakaojiunga na vyuo vya VETA kwa mwaka wa masomo 2026, kwa kutumia mfumo wa VETMIS.
Akishukuru kwa niaba ya watumishi waliopatiwa Mafunzo hayo Bi. Flaviana Minde, kutoka chuo cha VETA cha mkoa wa Mwanza amesema mafunzo hayo yawewatia moyo na kumwahidi Mkurugenzi Mkuu kwamba watakwenda kuboresha na kufikia kiwango tarajiwa katika utoaji mafunzo yanayohitajika.