The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Msaidizi wa Mkakuzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (AAG), Ali Zubery ameishauri Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuanzisha kampuni ya ujenzi baada ya kuonesha uwezo mkubwa wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyuo 25 vya ufundi stadi vya wilaya kwa kutumia mfumo wa nguvukazi ya ndani (yaani Force Account).
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake katika miradi ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya wilaya za Pangani, Mkinga, Korogwe na Kilindi, tarehe 26 Oktoba 2022, Zubery amesema katika ziara yake ya kukagua vyuo vinavyojengwa na VETA kwa kutumia Force Account, ameshuhudia majengo bora na ya kiwango cha juu, hivyo kushawishika kuishauri VETA kuanzisha kampuni ya ujenzi ili iweze kutoa huduma hiyo kwa upana zaidi.
“Kwa ujuzi wangu na uzoefu wa kukagua majengo ya serikali, naona ujenzi ni mzuri sana na wa kiwango cha juu. Nafikiri mnaweza kujenga majengo mengi zaidi hata ya taasisi zingine,” amesema.
Amesema utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa vyu vya ufundi stadi vya wilaya uliofanywa na VETA kwa kutumia mfumo wa nguvukazi ya ndani (Force account), utasaidia sana kuitangaza na kuiuza VETA katika eneo la uwezo wa ujenzi na kuifanya iaminiwe zaidi katika masuala ya ujenzi.
“Kutokana na ubora na uimara wa majengo haya, yataweza kusomesha vijana wa sasa na hata wajukuu wa vijana hao,” ameongoza.
Hata hivyo, Zubery ameishauri VETA kushughulikia suala la upatikanaji wa maji ya kutosha, ya uhakika na kutoka vyanzo vya kudumu katika vyuo vilivyojengwa, kwani licha ya ukubwa wa mahitaji katika vyuo husika, watu wengi wamesogea katika maeneo vilipojengwa vyuo, hivyo kuwa na uhitaji mkubwa wa maji kwa vyuo na jamii inayozunguka vyuo.
VETA imetekeleza mradi wa ujenzi wa vyuo 25 vya ufundi stadi vya wilaya za Korogwe, Pangani, Mkinga, Kilindi, Lushoto, Uyui, Igunga, Ikungi, Kishapu, Rufiji, Mafia, Ukerewe, Kwimba, Masasi, Ulanga, Mbarali, Chunya, Butiama, Uvinza, Iringa vijijini, Buhigwe, Chemba, Bahi, Monduli na Longido. Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo ulihusisha ujenzi wa majengo na utengeneza samani za vyuo hivyo.