The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
ABUNI LENSI, HADUBINI NA DARUBINI KWA KUTUMIA MAJI
Posted on: Thursday, 12 August 2021
Bellington Lyimo, mbunifu wa vifaa vya maabara aliye chini ya Kituo cha VETA cha Uatamizi wa Ubunifu na Ujasiriamali (VETA NICIE) amebuni lensi, hadubini na darubini kwa kutumia karatasi ngumu na maji kwa ajili ya kuchangia katika kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia masomo ya sayansi shuleni. VETA NICIE ni kituo kilicho chini ya usimamizi wa Chuo cha Walimu wa Ufundi Stadi Stadi Morogoro (MVTTC).
Akizungumza kwenye Maonesho ya Pili ya Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma leo, tarehe 29 Mei 2021, Lyimo amesema matumizi ya maji na karatasi ngumu ni mbadala wa glasi ambazo zinatumika katika kutengeneza vifaa hivyo ambavyo aghalabu ni vya gharama kubwa.
Akifafanua zaidi, Lyimo amesema kuwa vifaa vilivyobuniwa ni vya aina mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya walimu kufundisha na wanafunzi kujifunza kwa vitendo kanuni na tabia mbalimbali za mwanga, lensi, hadubini na darubini.
Amevitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni pamoja lensi za kufundishia kanuni na tabia za lensi; seti ya kufundishia tabia za mwanga kutoka mada moja kwenda nyingine; lensi kwa ajili ya kufundishia tabia za hadubini; lensi kwa ajili ya kufundishia tabia za darubini na kivunge kwa ajili ya kufundishia aina mbalimbali za lensi kama lensi mbonyeo na lensi mbinuko.
“Yote hii ni kwa ajili ya kuweka mbadala na kuongeza wigo wa elimu ya sayansi kwa vitendo na kuonesha kuwa tunaweza kutumia mada nyingine tofauti na glasi. Vilevile ni kurahisisha upatikanaji wa vifaa hivyo kwa gharama nafuu na kuhamasisha wanafunzi kufanya ubunifu kwa kutumia malighafi katika mazingira yanayowazunguka,” amesema.
Lyimo alianza ubunifu huo tangu mwaka 2010. Mwaka 2019 alishiriki Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) na kwenye kundi la Mfumo usio Rasmi, chini ya uratibu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na kuingia fainali.
Alipata ufadhili wa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kuendeleza huu ubunifu wake.
Anaendeleza ubunifu huo ikiwemo kuongeza ubora chini ya uatamizi wa VETA NICIE ambayo pia imesaidia kumkutanisha na walimu wa sekondari wanaofundisha masomo ya sayansi ambao wametoa mependekezo juu ya kuviimarisha zaidi.
Amesema pamoja na kufanya majaribio mbalimbali hadi kufikia hatua ya sasa katika katika ubunifu huo, lengo lake kufanya ubunifu mwingine zaidi unaolenga kusaidia ufundishaji wa masomo ya sayansi kwa vitendo.