The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Askari Polisi 95 mkoani Iringa wahitimu mafunzo ya udereva na ukaguzi wa magari
Posted on: Sunday, 09 February 2025
Askari Polisi 95 mkoani Iringa wahitimu mafunzo ya udereva na ukaguzi wa magari
Chuo cha VETA Iringa kimetoa mafunzo ya udereva na ukaguzi wa magari kwa jumla ya askari polisi 95 mkoani Iringa katika kipindi cha kuanzia Oktba 4 ,2023 hadi Novemba 22, 2024
Mafunzo hayo yaliyotolewa kwa awamu tatu yalikuwa na lengo la kuwawezesha askari wa ukaguzi wa magari kufanya kazi yao kwa weledi na kujiamini, ambapo awamu ya kwanza jumla ya askari 24 walihitimu, awamu ya pili askari 25 na awamu ya tatu askari 49 walihitimu nakufanya jumla ya askari 95 waliohitimu mafunzo hayo.
Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Iringa SACP, Bukumbi, akizungumza katika halfa ya kutunuku vyeti kwa wahitimu 49 wa mafunzo hayo, tarehe 10 Januari, 2025 katika chuo cha VETA Iringa, amesema askari wakipata ujuzi huo wataweza kufanya maamuzi sahihi na kujenga imani hata kwa madereva wanaowahudumia.
“Unamkamata na kumhoji wakati mwenyewe huna taaluma ya udereva, mafunzo haya yatatusaidia kufanya kazi kwa weledi,”. Amesema SACP Bukumbi.
Aidha SACP Bukumbi amesema kuwa wataanza kufuatilia wakaguzi wa magari wasio na taaluma ya udereva kwani hawataliwakilisha jeshi la polisi vizuri, na wametoa muda kwa kila askari wa usalama barabarani kupata mafunzo hayo.
Mmoja wa askari wa usalama barabarani waliopata mafunzo hayo ya udereva Daudi Henry amesema mafunzo hayo yata wasidiakupambana na kupunguza ajali za barabarani.
“Nitakapomkamata dereva kwa kuwa nimepata mafunzo nitajua gari lina ubovu, lakini pia nitajua wapi pa kukagua na hii imenipa nguvu zaidi wakati wa kukagua magari,” amesema Henry.
Naye Happiness Joseph ambaye pia ni miongoni mwa askari waliohitimu mafunzo hayo anasema watakuwa sambamba na madereva katika kufanya ukaguzi na kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha VETA Iringa, Pasiensi Nyoni, amewaomba wahitimu hao wa mafunzo ya udereva na ukaguzi wa magari kuwa mabalozi kwa madereva wengine nchini.
“leo tunao madereva wengi njiani abiria wakimshangilia anaongeza mwendo. Nawaomba mkawe mabalozi kwa madereva wengine kwani udereva sio kazi ya hovyo hovyo, udereva ni fani muhimu,” amesema.
Mafunzo hayo ni endelevu na yameanza kwa hizo awamu tatu kwa askari wa jeshi la polisi mkoani Iringa.