The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore amezindua rasmi Baraza Kuu la Wafanyakazi wa VETA, leo tarehe 20 Aprili, 2024.
Akizindua baraza na kikao chake cha kwanza katika Ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, CPA Kasore amewataka watumishi wanaounda baraza kuu la wafanyakazi wa VETA, kwenda kutekeleza jukumu kubwa la utoaji Mafunzo kwa weledi kwa ajili ya matokeo chanya yenye maslahi kwa VETA na Tanzania kwa ujumla.
Amewaomba wajumbe wa baraza kusaidia katika kuwawezesha Watanzania kunufaika na VETA, kufikia malengo pamoja na kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa na Watanzania wenye ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.
“ Tukaoneshe matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa VETA kupitia ujenzi wa vyuo kote nchini kwa kwenda kutekeleza wajibu wetu wa kutoa ujuzi unaokidhi viwango vinavyohitajika na wananchi ili kutimiza kiu na imani kubwa walio nayo kwetu katika kuwapitia Mafunzo” alihimiza.
Nae Mwakilishi wa Kamishna wa Kazi, Ndugu Honesta Ngolly amesema vipo vyama vya wafanyakazi kama RAAWU ambao wameaminiwa na watumishi wengine katika kuwawakilisha, hivyo uzinduzi wa baraza ukawape nafasi wawakilishi hao kukaa pamoja kujadili mustakabali wa wafanyakazi ili kuwapa moyo wa kuweza kuyatekeleza yale ambayo Tanzania inatarajia kutoka VETA.
Akishukuru kwa kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa wafanyakazi wenye mahitaji maalumu, Bakari Athumani, mwalimu wa fani ya Uungaji na Uundaji Vyuma kutoka VETA Kanda ya Ziwa, amewataka watumishi wanaoiwakilisha VETA kushirikiana na kuwa waadilifu katika kufanya kazi ili kuyafikia malengo ya Taasisi.
Baraza hilo litadumu katika kipindi cha miaka mitatu kulingana na mkataba wa uundaji wa mabaraza ya wafanyakazi uliosainiwa kati ya VETA na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Utafiti (RAAWU).