The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Bodi ya VETA yapongezwa uboreshaji na upanuzi wa utoaji mafunzo ya ufundi stadi nchini
Posted on: Tuesday, 10 January 2023
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael, ameipongeza Bodi ya Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa usimamizi thabiti wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuiaga Bodi hiyo jijini Dodoma tarehe 9 Januari, 2023, Dkt. Michael amesema miongoni mwa mambo yaliyosimamiwa vyema na Bodi hiyo ni ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya wilaya ambao umetekelezwa na VETA kwa kutumia nguvukazi ya ndani, pamoja na ubunifu wa programu za mafunzo kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na mwenendo wa nchi kiuchumi.
“Itoshe kusema kwamba usimamizi wenu ulikuwa mzuri na mmeitendea vyema mipango mbalimbali ya VETA, hasa Mpango Mkakati wa Tano (VCP V) wa mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023 ambao ndo hasa ulikuwa katika kipindi chetu cha usimamizi wa VETA… hongereni sana. ,” amesema.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeipa kipaumbele kikubwa sana elimu na mafunzo ya ufundi stadi na kwamba uendeshaji na usimamizi wake unapaswa kuwa imara na madhubuti.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, amesema katika kipindi cha kuanzia mwezi Februari, 2020, VETA imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo uandaaji wa mitaala 54 kuendana na mahitaji ya soko la ajira, uanzishwaji wa vyuo vipya 19 pamoja na utanuzi wa miundombinu 31 kwenye vyuo vya VETA nchini na kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vya VETA kutoka 56,000 mwaka 2020 hadi 141,854 mwaka 2023.
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Ndugu Peter Maduki, ameishukuru Serikali kwa kuiamini Bodi hiyo na kuipa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake na hatimaye kuiwezesha VETA kupiga hatua katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi.
Bodi ya Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ilianza kutekeleza majukumu yake tarehe 27 Februari, 2020 na inatarajiwa kumaliza muda wake tarehe 26 Februari 2023.