Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato (VETA Chato) umekamilika na tayari kimeshaanza kupokea maombi kwa ajili ya mafunzo ya kozi za muda mfupi yanayotarajiwa kuanza tarehe 5 Oktoba mwaka huu na kozi za muda mrefu yatakayoanza kutolewa Januari 2021.
Mkandarasi wa ujenzi wa chuo hicho, Kampuni ya C. F. Builders Ltd, alikabidhi rasmi mradi kwa Uongozi wa VETA tarehe 12 Septemba 2020 baada ya ujenzi wake kukamilika.
Chuo hicho kilichopo katika kijiji cha Itale, Kata ya Muungano, Tarafa ya Muungano, Wilayani Chato kilianza kujengwa Novemba mwaka 2018 na kimegharimu Shilingi za Kitanzania 10,713,316,360.57, ikijumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Baada ya kukamilika kwa chuo hicho, VETA imejipanga kuanza mafunzo mara moja na kwa hatua ya awali itaanza na mafunzo ya muda mfupi katika fani za Ubunifu wa Mavazi, Ushonaji na Teknolojia ya Nguo; Ufungaji na Utandazaji wa Bomba; Uashi; Huduma na Mauzo ya Chakula na Vinywaji; Uvuvi na Uchakataji wa Samaki na Uandaaji na Upishi wa Vyakula.
Fomu za kujiunga zimeshaanza kutolewa tangu tarehe 15 Septemba chuoni VETA Chato ambapo mafunzo ya muda mfupi (miezi mitatu) yanatarajiwa kuanza tarehe 5 Oktoba 2020 na ya muda mrefu Januari 2020.
Kwa kozi za muda mfupi ada ya masomoni kuwa kuanzia Shilingi 200,000 hadi 400,000 kwa miezi mitatu (3) kutegemeana na aina ya kozi na kwamba fomu zinatolewa kwa shilingi 5,000 tu. Tangazo la Kujiunga na Kozi za Muda Mfupi Katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato lililotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA tarehe 9 Septemba kupitia vyombo mbalimbali vya mawasiliano linaainisha vigezo na utaratibu mzima wa kujiunga na mafunzo hayo.
Baada ya vifaa na mahitaji mengine yote kukamilika, chuo cha VETA Chato kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 480 kwa mafunzo ya muda mrefu na wanafunzi wasiopungua 800 kwa mafunzo ya muda mfupi.
Licha ya chuo hicho kuwa wilayani Chato, kinatarajiwa kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa Mkoa wa Geita kwa ujumla kutokana na ukweli kuwa mkoa huo ulikuwa unakabiliwa na changamoto ya fursa chache za mafunzo ya Ufundi Stadi ambapo hadi mwaka 2019 kulikuwa na vyuo vya ufundi stadi vitatu tu vinavyomilikiwa na taasisi binafsi na za dini, vikiwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wasiozidi 300 kwa mwaka.
Kwa kutambua changamoto na uhitaji wa mkoa huo,VETA inajenga pia chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Geita katika eneo la eneo la Magogo mjini Geita.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amebainisha kuwa miongoni mwa fani zitakazotolewa katika chuo cha VETA cha Wilaya ya Chato ni Uandaaji Chakula na Huduma za Hoteli ili kukidhi mahitaji ya nguvukazi yenye ujuzi huo yanayotarajiwa kuongezeka kutokana na wilaya hiyo kuwa karibu na Hifadhi za Taifa za Burigi Chato na Rubondo.
Dkt. Bujulu anaitaja fani nyingine mahsusi kuwa ni Uvuvi na Uchakataji wa Samaki ili kusaidia katika kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao ya uvuvi na kupunguza upotevu mkubwa wa mazao ya samaki unaotokana na njia duni za utunzaji na uchakataji.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office