The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
DC NGORONGORO AITAKA VETA KUANZISHA KOZI ZA KILIMO, UFUGAJI NA UTALII
Posted on: Thursday, 08 December 2022
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Raymond Mwangwala, ameitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia chuo cha VETA cha Wilaya ya Ngorongoro kuanzisha fani za kilimo, ufugaji, hoteli na utalii ili kuwezesha wananchi wa Ngorongoro kupata stadi za kuboresha shughuli zao.
Akizungumza wakati wa mahafali ya kwanza ya chuo cha VETA Ngorongoro mkoani Arusha tarehe 2 Desemba, 2022, Mhe. Mwangwala amesema shughuli kubwa wanazofanya wananchi wa Ngorongoro ni za kilimo, ufugaji, hoteli na utalii hivyo wanahitaji mafunzo yatakayowapa ujuzi wa kuendesha shughuli hizo kitaalamu.
“Pamoja na kozi za ufugaji na kilimo, kozi zingine zinazohitajika wilayani hapa kuendana na shughuli za kijamii zinazozunguka chuo hiki (VETA Ngorongoro) ni za Utalii, hoteli na zile zinazohusiana na miundombinu ya maji,”amesema.
Aidha, Mhe. Mwangwala amepiga marufuku sherehe za bukwa zinazohususisha wazazi kuwaozesha wanafunzi na kuwataka wananchi wa Ngorongoro kuchangamkia fursa za mafunzo ya ufundi stadi.
DC Mwangwala ameagiza wadau mbalimbali kushirikiana na chuo hicho katika kuwezesha upatikanaji wa magari ya kuendesha kozi za udereva.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kaskazini, Bi. Monica Mbelle, aliwasihi wananchi kutumia fursa za mafunzo zinazopatikana kwenye vyuo vya VETA kwenye kanda hiyo kujipatia ujuzi utakaowasaidia katika kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Bi. Mbelle alisema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa magari ya kufundishia kozi za udereva na kumuomba mgeni rasmi kusaidia upatikanaji wa magari ili kutatua changamoto hiyo.
Mkuu wa Chuo cha VETA Ngorongoro, Ndugu Gabriel Sikoi, alisema chuo hicho kilipokelewa kutoka kwa wananchi kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mwaka 2019 na VETA ilifanya ukarabati na ukamilishaji wa majengo hayo na kuanza kutoa mafunzo mwezi Januari, 2021.
Awamu ya pili ya ujenzi inahusisha ujenzi wa mabweni mawili, bwalo la chakula, madarasa mawili, nyumba ya watumishi ya familia mbili ambapo ujenzi umefikia asilimia 81.
Ndugu Sikoi alitaja baadhi ya changamoto zinazokabili chuo hicho kuwa ni mwamko mdogo wa jamii inayozunguka chuo kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi na ukosefu wa magari ya kuendeshea kozi za udereva.
Mahafali ya kwanza ya Chuo cha VETA Ngorongoro imehusisha wahitimu 47 (wavulana 29 na wasichana 18) katika fani za umeme wa majumbani, uashi na ushonaji. Wanafunzi wengine 89 (wavulana 53 na wasichana 36) wanaendelea na masomo chuoni hapo.