The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
KKKT kuanzisha chuo cha ufundi stadi kwa wenye ulemavu wa akili
Posted on: Tuesday, 07 September 2021
Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), liko mbioni kuanzisha chuo maalum cha ufundi stadi kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa akili katika eneo la Mlandizi, mkoani Pwani.
Naibu Katibu Mkuu wa DMP anayeshughulikia Huduma za Jamii, Bi. Agnes Lema, alibainisha hayo Jumatano, tarehe 1 Septemba 2021, katika kikao cha mashauriano na Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kilichofanyika kwenye ofisi za VETA Makao Makuu, jijini Dodoma.
Amesema mpango huo wenye lengo la kujenga fursa za ajira kwa watu wenye ulemavu wa akili nchini Tanzania ulianza tangu mwaka 2012 na matayarisho kuanza rasmi mwaka 2017. Kwa sasa matayarisho hayo yamefikia hatua nzuri na hivyo wamedhamiria kuhakikisha mafunzo yanaanza rasmi mwaka ujao, 2022.
“Kwa kweli sisi tunaomba ushirikiano wenu katika nyanja zote. VETA mtupe miongozo, ushauri, mitaala na kila kitu ambacho kitasaidia kuwezesha mpango huu wa kusaidia vijana hawa kupata mafunzo unafanikiwa” amesema Bi. Lema.
Akitoa wasilisho kuhusu Chuo hicho na mpango wa mafunzo, Mratibu wa Mradi wa Mradi huo, Bi. Caroline Shedafa amesema kuwa wazo la kuanzisha chuo cha ufundi stadi kwa watu wenye ulemavu wa akili lilianza mwaka 2012 kutokana na uzoefu wa karibu miaka 40 ya utoaji elimu ya shule ya msingi kwa watu wenye ulemavu wa akili na usonji, katika kituo cha Kanisa hilo kijulikanacho kama “Mtoni Deacon Lutheran Centre”, kilichoko Mtoni jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kinaendeshwa na Kanisa hilo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
“Changamoto ni kwamba, wanafunzi wengi wenye ulemavu wa akili na wanaosoma Kituo cha Mtoni, baada ya kumaliza masomo yao, wanakosa mahali pa kwenda, kwani hakuna fursa ya kuendelea na masomo ili kuendeleza ujuzi na stadi walizopata kituoni hapo au katika vituo vingine ya aina hiyo. Hivyo, vijana hawa hushindwa kupata ajira au kujiajiri. Kwa hiyo, vijana hawa hukaa tu nyumbani bila shughuli maalum na kuendelea kuwa wategemezi,” amesema.
Bi. Shedafa amesema Chuo cha Ufundi Stadi kwa Watu wenye Ulemavu wa Akili Mlandizi kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 200 wa bweni na kitatoa kozi mbalimbali zikiwemo Utunzaji wa Nyumba, Uandaaji Chakula, Upishi na Uokaji Mikate.
Ameongeza kuwa wanafunzi watapewa fursa ya kwenda kufanya mazoezi ya kazi wakati wakiwa chuoni ili kuanza kuwaandaa kwa kazi husika.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu ameipongeza Dayosis ya Mashariki na Pwani ya KKKT kwa mpango huo, kwani vijana wengi wenye ulemavu wa akili wamekuwa na fursa finyu katika mafunzo ya ufundi stadi, ingawa wakipata mafunzo hayo wanaonekana kuyamudu na kufanya vyema.
Ameahidi kuwa VETA itasaidiana na Kanisa kwa karibu sana katika hatua mbalimbali za uanzishaji wa chuo hicho kwa kutoa miongozo na ushauri ili maandalizi yote yakamilike tayari kwa chuo kusajiliwa na kuanza mafunzo kama inavyotarajiwa.