Magufuli apongeza jitihada zinazofanywa na VETA kupanua mafunzo ya ufundi stadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli jana Aprili, 5 2019 amezindua Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma huku akiupongeza uongozi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA) kwa jitihada zake katika kupanua fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Akihutubia wananchi baada ya uzinduzi katika eneo la chuo hicho, Rais Magufuli alisema kuwa VETA imeweza kujenga vyuo vingi katika kipindi kifupi sambamba na kubuni namna zingine za kupanua fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi. “mmejenga vyuo vingi, hilo ni lazima niseme kwa dhati, kila mahali sasa kuna vyuo vingi vinajengwa na mmejitahidi katika kipindi kifupi,” alisema.
Alizitaja jitihada zingine zilizofanywa kuwa ni pamoja kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo na mafunzo ya uanagenzi yanayohusisha vyuo na mahala pa kazi hivyo kusaidia vijana kupata muda mwingi wa mafunzo kwa vitendo.
Aliwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika kipindi hiki akieleza kuwa nchi ya Tanzania sasa inaelekea kwenda kwenye uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda na hivyo inahitaji nguvukazi yenye ufundi stadi ambayo huandaliwa na vyuo vya ufundi stadi vikiwemo vyuo vya VETA.
Hata hivyo, Rais Magufuli aliiagiza VETA kufikiria juu ya kupunguza gharama za ujenzi na ukarabati wa vyuo kwa kutumia nguvukazi ya ndani. “Inawezekana siku nyingine mnaweza kujifunza kwa kujenga kwa force account (nguvu ya ndani).
Mkaichukua kama emergency (dharura) na kama trial (majaribio) ya VETA yenyewe, mkawapa hawa vijana wa VETA na ninyi mkawa consultants (washauri elekezi). ………….Na mimi nitawalinda kama kukitokea audit query (hoja ya ukaguzi),” alisema. Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknojolia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako katika maelezo yake kabla ya kumkaribisha Rais alieleza kuwa taratibu za ununuzi wa vifaa kwa ajili ya chuo cha VETA Namtumbo zinaendelea ikiwemo utengenezaji wa samani ambao unafanywa na Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA Mbeya.
Alisema chuo hicho kinatarajiwa kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi katika fani za Ufundi wa Maabara; Compyuta; Uashi; Umeme wa majumbani na Vifaa vya Umeme (Electronics), Ufundi Bomba; Ushonaji; Useremala na ufundi wa Mitambo Mizito. Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, Chuo hicho kina uwezo wa kudahili wanafunzi 900 kwa mwaka ambapo wanafunzi 175 ni wa mafunzo ya muda mrefu kwa ngazi ya kwanza na wanafunzi 175 kwa ngazi ya pili na 600 wa mafunzo ya muda mfupi.
Awali baada ya kupewa fursa kuzungumza, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Mhe. Juma Nkamia aliupongeza uongozi wa VETA kwa kazi nzuri na kuahidi kuwa kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi wa VETA, Kamati yake itakuwa tayari kuidhinisha fedha mara moja muda wowote ikitokea kuna maombi ya fedha kwa ajili ya shughuli za VETA.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office