The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
MHE.MAVUNDE AWASIHI WAAJIRI KUWEKEZA KWA WAHITIMU WA UFUNDI STADI NCHINI.
Posted on: Thursday, 24 August 2023
MHE.MAVUNDE AWASIHI WAAJIRI KUWEKEZA KWA WAHITIMU WA UFUNDI STADI NCHINI.
Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Anthony Mavunde amewasihi Waajiri kuwapatia fursa za ajira vijana waliohitimu Mafunzo ya Ufundi Stadi katika vyuo mbalimbali vya VETA nchini kupitia mradi wa kukuza Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo Afrika(E4D).
Mhe. Mavunde ametoa wito huo leo tarehe 24.08.2023 alipokuwa akifungua Kongamano la Ujuzi na Ajira lililofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma lililoandaliwa na VETA kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani(GIZ).
Amesema kuwa vijana ni rasilimali muhimu na nguvu kazi yenye kuleta mabadiliko na kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu,hivyo wakipatiwa fursa ya kutumia ujuzi wao wanaweza kukuza uchumi wa familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Mhe Mavunde amesisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali nchini kuboresha upatikanaji wa mitaji na mikopo kwa vijana na wajasiriamali ili kuweka mazingira rafiki ya kuendeleza shughuli zao.
“Tunahitaji kuwekeza katika miundombinu bora ya elimu ya mafunzo bila kusahau kuweka mazingira rafiki ya biashara na ajira kwa vijana wetu,”amesema
Akitoa taarifa fupi ya Utekelezaji wa Mradi wa E4D,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA,CPA Antony Kasore amesema,VETA inajivunia mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo na itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha miundombinu ya utoaji Mafunzo na kuandaa programu za Ufundi Stadi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira.
CPA Kasore amesema mradi wa E4D umenufaisha jumla ya vijana 3,258 katika fani za Ufundi Bomba wa Majumbani, Ufundi Bomba Viwandani na Ufundi wa Uchomeleaji Vyuma Viwandani (Industrial Welding) katika vyuo vya VETA vya Dodoma, Lindi na Manyara.
Kwa upande wake, Meneja Miradi kutoka GIZ Ndg.Awadh Milasi amesema utekelezaji wa programu hiyo umekuwa na mafanikio kwa kuwa umewezesha vijana kujipatia ujuzi na baadhi yao wameweza
kuajiriwa na wengine kujiajiri.
Kongamano la Ujuzi na Ajira (Job and Skills Fair) lenye kauli mbiu isemayo “Ufundi Stadi kwa Fursa zaidi za Ajira” lilifanyika kwa lengo la kuwajengea wananchi uelewa juu ya fursa za Ufundi Stadi zitolewazo kupitia mradi wa E4D, kukuza uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa wanufaika wa kozi zilizotolewa katika vyuo vya VETA nchini chini ya mradi huo.