The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mkurugenzi Mkuu VETA ahimiza uzalishaji katika vyuo vya VETA
Posted on: Thursday, 07 November 2024
Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA, Anthony Kasore, amehimiza vyuo vya VETA hapa nchini kufanya shughuli za uzalishaji sambamba na utoaji mafunzo.
CPA Kasore ameyasema hayo tarehe 5 Novemba 2024, alipotembelea vyuo vya VETA Wilaya za Kasulu, Uvinza na Ulyankulu, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea vyuo vya VETA vilivyopo katika Kanda ya Magharibi.
Akiwa katika vyuo hivyo CPA Kasore amesema pamoja na kuendelea kuimarisha mafunzo, VETA inaongeza mikakati na juhudi uzalishaji ili kupanua wigo wa mapato.
"Katika kuhakikisha hilo linatekelezwa tumefungua kampuni tanzu ijulikananyo kama Ujuzi Incorporated Company limited ambayo itakuwa ikijihusisha na kubiasharisha bidhaa zinazotengenezwa na huduma zinazotolewa kupitia mafunzo ya ufundi stadi," amesema CPA Kasore.
Kasore amesema kampuni hiyo kwa sasa imeshasajiliwa na taratibu za kuanza kufanya kazi zinakamilishwa.
Amesisitiza vyuo hivyo kutumia fursa hiyo ya kuwepo kwa kampuni kufanya uzalishaji kwa wingi.
Amesema kwa kupitia kampuni hiyo, wafanyakazi wa VETA watapatiwa motisha, kwani kiasi cha faida itakayokuwa inapatikana katika kampuni hiyo itakuwa ikienda kwa wafanyakazi kama motisha na nyingine kuichangia Serikali katika matumizi yake.
Akiwa katika vyuo hivyo amepata nafasi ya kutembelea karakana kujionea shughuli mbalimbali za utoaji mafunzo na kuongea na walimu na wanafunzi na kuwafahamisha uwepo wa kampuni hiyo utasaidia VETA kuingiza mapato na kupunguza utegemezi kwa Serikali