The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
MKURUGENZI MKUU VETA AWAASA WATUMISHI KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO SAMBAMBA NA IMANI YA RAIS KWA TAASISI
Posted on: Friday, 02 May 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amewaasa watumishi wa Mamlaka hiyo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa bidii na ufanisi, ili kufikia matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa wakati huu ambapo Rais ameendelea kuonyesha imani kubwa kwa VETA.
CPA Kasore alitoa wito huo wakati wa mkutano wa pamoja wa watumishi wa VETA uliofanyika katika chuo cha VETA Singida, mara baada ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika Kitaifa mkoani humo, tarehe 1 Mei 2025.
Tukio hilo lilihusisha uwakilishi wa watumishi kutoka Makao Makuu ya VETA pamoja na vyuo vya Kanda ya Kati ambavyo ni Manyara, Simanjiro, Gorowa, Bahi, Chemba, Dodoma na Kongwa.
“Kila mtu atekeleze majukumu yake kwa kiwango cha juu, kila mtu atoe huduma kwa kiwango cha juu, ili kufikia matarajio ya Mheshimiwa Rais kwetu,” amesema CPA Kasore.
Amefafanua kuwa uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita kujenga vyuo 65 vipya vya VETA katika wilaya mbalimbali ni ushahidi wa wazi wa imani kubwa ya Rais kwa mchango wa VETA katika maendeleo ya Taifa.
Aidha, amewataka watumishi kufanya kazi kwa mshikamano, kuepuka makundi yasiyo rasmi kazini ambayo yanaweza kudhoofisha taasisi, na badala yake kila mmoja ahusike kujenga mazingira rafiki na salama kwa wengine.
“Tusitengeneze mazingira ya kuwafanya wenzetu kuiona ofisi kama mahala pagumu na kuichukia,” ameonya.
Pia ameeleza kuwa utekelezaji wa Mpango wa Motisha kwa watumishi umeanza rasmi kupitia kipengele cha posho za safari, na akahimiza kuongeza juhudi za uzalishaji ili kuwezesha utekelezaji wa vipengele vingine vilivyobaki katika mpango huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, Ramadhani Mataka, amependekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa kuwa na tukio rasmi la Mei Mosi kwa sura ya VETA kitaifa.
Amesema kuwa kila mwaka, wawakilishi wa Makao Makuu, kanda na vyuo wakutane katika mkoa ambako maadhimisho ya kitaifa yanafanyika, ili kutumia siku hiyo kama fursa ya kutathmini utekelezaji wa majukumu, mafanikio na changamoto za kitaasisi.
Amesisitiza kuwa utaratibu huo utasaidia kuimarisha umoja, kujadiliana masuala ya msingi ya utendaji na kupanga kwa pamoja mikakati ya kuongeza ufanisi na tija katika kazi.
Katika tukio hilo pia, mtumishi Marco Amani Mhanze alitunukiwa tuzo ya Mfanyakazi Bora wa VETA kwa mwaka 2024, ikiwa ni kutambua juhudi zake, maadili na ubunifu aliouonyesha katika kutekeleza majukumu yake. Tukio hilo la utoaji tuzo limeibua hamasa kwa watumishi wengine kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa maslahi ya taasisi na Taifa kwa ujumla.