The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mkurugenzi Mkuu wa VETA akagua hali ya utoaji mafunzo chuo cha VETA Kigoma
Posted on: Wednesday, 06 November 2024
Tarehe 4 Novemba 2024 Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, akiwa ameambatana na Menejimenti ya VETA amefanya ziara katika chuo cha VETA Kigoma kukagua hali ya utoaji mafunzo chuoni hapo.
Miongoni mwa maeneo aliyoyakagua ni karakana ambazo ndio msingi wa utoaji mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA.
Aidha akiwa chuoni hapo CPA Kasore amezungumza na walimu pamoja na uongozi wa chuo hicho na kuwaeleza kuwa nia ya Serikali ni kuona watanzania wenye uhitaji wa kupata elimu n a mafunzo ya ufundi wanapata katika ubora wa hali ya juu.
“Tunapaswa kutoa mafunzo haya ya ufundi stadi katika viwango bora ili mwisho wa siku wale watakaopata ujuzi huo waweze kujiajiri au kuajiriwa pindi wanapohitimu mafunzo, " amesema CPA Kasore.
Sambamba na hilo Mkurugenzi Mkuu VETA amewakumbusha walimu na watumishi chuoni hapo kutoa ushirikiano katika shule za sekondari ambazo zina jukumu la kutoa mafunzo ya amali hapa nchini.
“Tuzingatie nia ya Serikali ya kufanya mabadiliko katika Sera ya Elimu kupitia hii elimu ya amali tuhakikishe wanapohitaji kujifunza kupitia karakana basi ziwe wazi muda wote na walimu mtakapohitajika kwenda huko kufundisha basi muwe tayari,” amesisitiza CPA Kasore.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi VETA, Kanda ya Magharibi, Nyongo Kihenge amesema katika kanda hiyo kuna jumla ya vyuo 22 kati ya hivyo vyuo 14 vimeanza kutoa mafunzo na vyuo 8 vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Kigoma, Paul Kimenya, amesema watafanyia kazi maelekezo yote ya Mkurugenzi Mkuuu .
Ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA ya kukagua vyuo vya VETA hapa nchini imeanzia Kanda ya Magharibi na itaendelea katika Kanda zingine.