The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
MKURUGENZI MKUU WA VETA ASISITIZA USHIRIKIANO BAINA YA WAFANYAKAZI KUIMARISHA UTOAJI MAFUNZO
Posted on: Monday, 15 April 2024
MKURUGENZI MKUU WA VETA ASISITIZA USHIRIKIANO BAINA YA WAFANYAKAZI KUIMARISHA UTOAJI MAFUNZO YA UFUNDI STADI
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amewataka wafanyakazi wa VETA kuboresha ushirikiano katika utendaji kazi ili kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
CPA. Kasore ametoa wito huo tarehe 14 Aprili, 2024 katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dodoma wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na watumishi hao ya kumpokea na kumpongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA.
Amesema ushirikiano baina ya wafanyakazi wa Mamlaka hiyo utawezesha ufanisi katika kutekeleza shughuli za utoaji mafunzo hasa kwa kutambua umuhimu na mchango wa kila mmoja katika kufikia malengo yaliyowekwa.
CPA Kasore amesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha malengo ya Serikali ya kutoa ujuzi kwa Watanzania kupitia vyuo vya VETA nchini yanafikiwa na kuwataka watumishi wa VETA kushiriki kikamilifu katika kuweka mipango na mikakati thabiti ya kufanikisha dhamira hiyo ya Serikali.
“Nasisitiza wote (watumishi) kutambua jukumu kubwa tulilonalo katika kuwapatia wananchi ujuzi ambao ndiyo msingi mkuu katika kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi zitakazowaongezea kipato na kuongeza pato la taifa kwa ujumla …Ni wajibu wetu kufanikisha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa ubora na umahiri,”amesema
Awali, Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Abdallah Ngodu amempongeza CPA Kasore kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mhe. Rais na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji mafunzo ya ufundi stadi zinazofanywa na VETA.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa VETA, Mtunza Kumbukumbu wa VETA Makao Makuu, Hussein Rubaka amempongeza CPA. Kasore kwa kuteuliwa kuiongoza VETA na kuahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake huku wakifanya kazi kwa kujituma na kwa ufanisi ili kufikia malengo la Taasisi.
CPA Anthony Kasore aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, tarehe 12 Aprili, 2024 . Kabla ya uteuzi huo, CPA Kasore alikuwa akikaimu nafasi hiyo.