The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Antony Kasore amewahimiza wafanyakazi wa VETA kufanya kazi kwa amani
Posted on: Sunday, 09 February 2025
Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Antony Kasore amewahimiza wafanyakazi wa VETA kufanya kazi kwa amani, upendo na umoja ili kufikia malengo ya mwaka 2025.
CPA Kasore amesema hayo leo tarehe 31 Desemba 2024 alipokuwa akitoa salamu za kufunga mwaka 2024 na kupokea mwaka 2025 kwa watumishi wa VETA Makao Makuu Jijini Dodoma, wakiwawakilisha watumishi VETA kote nchini.
“Katika kutekeleza majukumu yetu sisi VETA tunatakiwa kuhakikisha watanzania wanapata ujuzi ili waweze kujiajiri au kuajiriwa ili kuwawezeshakujipatia kipato chao cha kila siku kutokana na ujuzi walioupata VETA na hilo litawezekana kama tutakuwa na nia moja katika kutimiza malengo yetu” amesema CPA Kasore.
Aidha Mkurugenzi Mkuu amesema matarajio ya Watanzania wengi ni kuona mafunzo ya Ufundi Stadi yanayotolewa VETA yanawasaidia kuwatoa katika maisha ya kawaida.
Sambamba na hilo CPA Kasore amewataka watumishi wa VETA kote Nchini kuendelae kufanya kazi kwa nguvu, jitihada na ari.
Amesisitiza kuwa kila idara na mtumishi wa VETA ana malengo yake, na hivyo ni muhimu kuhakikisha malengo haya yanatimizwa.
Ameeleza mafanikio ya mwaka 2024, akisema kuwa idadi ya vyuo vya VETA imeongezeka na ujenzi wa vyuo 65 unaendelea, huku lengo la kufikia vyuo 145 ifikapo mwaka 2025 likiendelea kutekelezwa.
CPA Kasore amesisitiza pia umuhimu wa kutoa mafunzo ya amali kwa wanafunzi wa sekondari ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
CPA Kasore amehitimisha salamu zake za mwaka mpya kwa kutoa shukurani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA mwezi Aprili 2024.
Alisema kuwa ushirikiano na umoja kati ya VETA na Bodi yake, inayoongozwa na Profesa Sifuni Machome, umeleta mafanikio makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja.