The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti ahamasisha vijana kuchangamkia fursa za mafunzo kwenye chuo cha VETA Rufiji
Posted on: Wednesday, 10 July 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti ahamasisha vijana kuchangamkia fursa za mafunzo kwenye chuo cha VETA Rufiji
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Mhe. Kanali Joseph Kolombo, amewahamasisha vijana wa Wilaya ya Rufiji kujitokeza kwa wingi kupata mafunzo ya ufundi stadi kwenye chuo kipya cha VETA Rufiji.
Kanali Kalombo ametoa wito huo tarehe 8 Julai, 2024 Wilayani Rufiji
akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja. Edward Gowele wakati
wa zoezi la uhamasishaji kwa wananchi kujiunga na Chuo cha VETA Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ambacho ni miongoni mwa vyuo 25 vya VETA ngazi ya Wilaya vilivyojengwa na Serikali kuanza kutoa mafunzo mwaka 2023.
Amesema nia ya Serikali kuwaletea chuo hicho ni kuwasogezea wananchi fursa za mafunzo ya Ufundi Stadi karibu nao na hatimaye wapate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
”Tunataka hata wakija wawekezaji katika maeneo yetu wasiwe na tabu ya kutafuta vijana wenye ujuzi,’’ amesema
Amesema viwanda vingi vinaendelea kujengwa katika Mkoa wa Pwani hivyo ni wajibu wa wananchi mkoani hapo kujiandaa kutumia fursa za ajira zitakazojitokeza na kwamba wasipofanya hivyo wananchi wa mikoa ya jirani watachangamkia fursa hizo.
Mhe. Kalombo ameahidi kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na chuo hicho na kuiweka kama ajenda katika vikao wilayani hapo.
Naye Mkurugenzi wa VETA kanda ya Mashariki, John Mwanja, alitoa shukrani kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha ujenzi wa vyuo na kupanua fursa za mafunzo kwa wananchi.
Amesema VETA imejipanga vyema kutoa mafunzo ya ufundi stadi chuoni hapo na kuwahimiza wanaRufiji kujitokeza.
Kwa upande wake Msajili wa chuo hicho, Julius Mkasasa alisema Chuo cha VETA Wilaya ya Rufiji kipo katika Kijiji cha Nyanda Utunge katika Halmashauri ya mji mdogo wa Utete na Kipo umbali wa kilomita 12 kutoka ofisi ya Wilaya ya Rufiji.
Alitaja fani zinazotolewa kwenye chuo hicho kuwa ni Ujenzi, Uundaji na Uungaji vyuma, Ubunifu na Ushonaji wa Mavazi, Uhazili na Kompyuta, Ufundi Umeme wa Majumbani, Ufundi Magari, Kompyuta, Ufundi bomba, Udereva wa pikipiki na Bajaji, Ujasiriamali, Ufugaji na Kilimo ambazo hutolewa kwa muda mrefu na muda mfupi.