The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
MVTTC yatakiwa kupanua wigo wa mafunzo kukabiliana na ongezeko la mahitaji
Posted on: Wednesday, 03 April 2024
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt Franklin Rwezimula, amekitaka Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kupanua wigo wake wa udahili na kuboresha utoaji wa mafunzo ili kiweze kuwa kituo mahsusi cha kutoa walimu mahiri na wa kutosha kwa ajili ya vyuo vya ufundi stadi vinavyoendelea kujengwa nchini, pamoja na wakufunzi wa karakana (workshop instructors) kwa ajili ya shule za sekondari za amali.
Dkt. Rwezimula ametoa wito huo wakati wa mahafali ya 26 ya MVTTC, tarehe 22 Machi, 2024, iliyowahusisha walimu tarajali 218 wa ualimu wa ufundi stadi kwa ngazi ya Astashahada na Shahada.
Dkt Rwezamula ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, amesisitiza umuhimu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika utekelezaji wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Elimu kwa kuhakikisha Watanzania wanapata ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kujiajiri na kukuza uchumi wa Taifa.
Amesema wahitimu wao pia watachangia katika kuwezesha utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo Toleo la 2023 kuhusu mafunzo ya amali ambapo walimu mahiri wanatakiwa ili kutoa mafunzo hayo kwa ufanisi.
“Nguvu kazi yenye ujuzi itahitajika sana katika miradi ya kimkakati kama vile uzalishaji wa nishati, uchimbaji wa madini ya kimkakati, ujenzi wa bomba la mafuta na ujenzi wa reli ya kisasa. Miradi yote hii itahitaji mafundi mahiri watakaozalishwa na ninyi……,” amesema.
Dkt. Rwezimula amewataka wahitimu hao kutambua na kutimiza vyema wajibu walionao katika kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi unaohitajika katika utekelezaji wa shughuli za kiuchumi na miradi ya kimkakati.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha MVTTC, Samweli Kaali, amebainisha kuwa miongoni mwa vipaumbele vya chuo hicho ni kuimarisha uwezo ili kiweze kukidhi mahitaji ya walimu kufuatia ongezeko la vyuo vya ufundi stadi nchini pamoja na mabadiliko ya Sera ya Elimu na mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023.
Amesema chuo hicho kimejipanga kuongeza udahili wa walimu tarajali kutoka walimu 1500 hadi kufikia walimu 3100 ifikapo Juni 2028, sambamba na uanzishaji wa mitaala mipya 18 ya Stashahada za Ualimu wa Ufundi na Ufundi Stadi ngazi ya 4 hadi 6 (NTA Level 4-6) katika fani sita za Kisekta ambazo ni Ujenzi, Magari, Umeme, Makenika ya Mitambo, Sanaa Bunifu na Usindikaji Chakula.