The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mwenyekiti wa Bodi ya VETA ahimiza mawazo ya ujasiriamali katika mafunzo ya ufundi stadi
Posted on: Sunday, 09 February 2025
Mwenyekiti wa Bodi ya VETA ahimiza mawazo ya ujasiriamali katika mafunzo ya ufundi stadi
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board), Prof. Sifuni Mchome, amewataka watendaji wa VETA kubadilisha fikra katika utoaji wa mafunzo kwa kuzingatia mbinu za ujasiriamali na kuimarisha uzalishaji katika vyuo vya ufundi stadi.
Prof. Mchome aliyasema hayo leo, tarehe 31 January 2025, katika kikao kilichohusisha Menejimenti ya VETA Makao Makuu, Wakurugenzi wa Kanda, na Wakuu wa vyuo vya VETA nchini, katika ukumbi wa Mt. Gaspar, jijini Dodoma.
Katika hotuba yake, Prof. Mchome amesisitiza kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanalenga maandalizi ya wahitimu kwa ajili ya kazi halisi badala ya nadharia pekee.
Ameeleza kuwa vyuo vya VETA vina fursa kubwa ya uzalishaji na vinapaswa kufundisha stadi zinazotatua mahitaji ya ujuzi katika jamii inayovizunguka.
Akitoa mfano wa mkoa wa Dodoma, amehimiza kutumia ujuzi na teknolojia ya ndani kuongeza thamani ya zao la zabibu badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa mafunzo kwa vitendo kwa kutumia mazingira halisi ya kazi, akitolea mfano wa wanafunzi wa uashi kutumika kwenye miradi halisi ya ujenzi, huku wale wa ufundi magari wakifundishwa kwa kutumia magari halisi badala ya vifaa vya mafunzo vya mfano.
Kwa kufanya hivyo, amesema, viwango vya ujuzi vitaimarika na kuwa na wahitimu waliobobea kwenye stadi zao.
Kuhusu ubunifu, Prof. Mchome ameeleza kuwa jitihada za wabunifu zinapaswa kuelekezwa kwenye kuingiza bidhaa sokoni badala ya kuishia kwenye maonyesho.
“Ubunifu uwe siri hadi ufikie hatua ya kuuzwa ili kulinda na kuongeza thamani yake,” amesema .
Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amezungumzia juhudi za Mamlaka hiyo katika utoaji mafunzo ya ufundi stadi ikiwemo ongezeko la udahili wa wanafunzi, maboresho ya mitaala mbalimbali, ununuzi wa vifaa vya kisasa kwenye karakana, kufanikiwa kubiasharisha ubunifu wa aina 14 na kuanzisha kampuni ambayo itatumika kufanya shughuli mbalimbali za kibiashara.
Ameishukuru VET Board kwa usimamizi mzuri ambao umewezesha utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo, na kusema kuwa juhudi zinaiwezesha VETA kuzidi kuwa chachu ya maendeleo ya ujuzi na ajira nchini.